SERIKALI YAUCHOMOA MUSWADA WA MAHAKAMA YA KADHI BUNGENI

0 coment

Serikali imeuchomoa muswada wa kuanzisha
Mahakama ya Kadhi uliokuwa uwasilishwe
bungeni ili yafanyike maridhiano kwanza.
Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, taasisi 11 za
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimeazimia
kuwahamasisha wana jumuiya wake kususia Kura
ya Maoni ya Katiba Mpya hadi watakapopata
uhakika wa kuwa na Mahakama ya Kadhi yenye
meno.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala iliyokutana
jana mjini Dodoma ilielezwa kuwa Serikali
imeomba muda wa kufanya maridhiano kabla ya
kuwasilishwa muswada huo katika mkutano huu
wa Bunge unaomalizika kesho. Ilielezwa kuwa
muswada huo utawasilishwa katika mkutano ujao
wa Bunge.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo
zinasema kuwa Bunge liliamua kuondoa
muswada huo kujadiliwa pamoja na sheria
mbalimbali na badala yake ujadiliwe peke yake.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa
Muhambwe, Felix Mkosamali alisema katika kikao
chao Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jasson Rweikiza
aliwaeleza kuwa Serikali imeomba hivyo ili
kufanya maridhiano na kuahidi kuwa
itauwasilisha katika mkutano wa Bunge ujao.
Taasisi zapinga
Kauli ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zipatazo 11
iliyotolewa Dar es Salaam jana na kusomwa na
Naibu Katibu wa Jumuiya ya Shura ya Maimamu,
Sheikh Rajabu Katimba ilisema itasusia mchakato
wa Kura ya Maoni kwa madai kuwa
kinachoendelea katika mchakato wa kupatikana
kwa Mahakama hiyo ni hadaa za Serikali
zinazofanyika miaka yote hasa kinapofika kipindi
cha kupiga kura kwa lengo la kuungwa mkono
na waumini hao.
Akizungumza kwa niaba ya jumuiya hizo
zikiwamo, Baraza Kuu, Tampro, Basuta, Jasuta, IPC,
Haiyat Ulamaa na Shura ya Maimamu Tanzania,
Sheikh Katimba alisema watawahamasisha
Waislamu wanaounda Jumuiya hizo kutopiga kura
ya maoni wala kushiriki kwa namna yoyote ile
katika mchakato wa kupatikana Katiba Mpya kwa
sababu haiitambui Mahakama hiyo.
Alisema mchakato wa kutoa maoni juu ya
muswada unaohusu Mahakama ya Kadhi
umepotoshwa kwa kuituhumu kuwa italeta
vurugu ikiwamo kuhukumu kwa kukata watu
mikono, kuhukumu wasiokuwa Waislamu na
kuwabagua wasiokuwa Waislamu na kwamba ni
upotoshaji wa makusudi ukiwa na lengo la hadaa.
“Wamefanya hivyo makusudi ili wananchi na
Serikali wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na
taasisi 11, ambayo kama yatafanyiwa kazi na
Serikali yatawezesha kupatikana kwa Mahakama
ya Kadhi inayokidhi matakwa ya Sheria za Kiislamu
na wajibu wake kama mamlaka ya kutoa na
kutenda haki,” alisema Sheikh Katimba.
Hata hivyo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa
Shaaban Simba alisema Kamati ya kudumu ya
Bunge ya Katiba Sheria na Utawala ilipata maoni ya
taasisi zote za Kiislamu na kila moja ilitoa maoni ya
nini kifanyike ili kuboresha muswada wa
Mahakama ya Kadhi.
Alisema Bakwata iliungana na Serikali na
kukubaliana nini kitoke, kibaki, kiboreshwe na
kusema taasisi hizo nazo zilipaswa kutumia wakati
huo kukubali, kukataa, kutoa mapendekezo,
kujadili.
Muswada huo ulitarajiwa kuzua mjadala mkali
hasa baada ya Jukwaa la Wakristo Tanzania
kuitaka Serikali kuachana nao ili kuepusha
kuvunja misingi ya Taifa inayopinga ubaguzi na
kutofungamana na dini yoyote.
Suala hilo lilikuwamo katika Muswada wa
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali uliotarajiwa
kuwasilishwa bungeni wiki hii na ulilenga kufanya
mabadiliko katika Sheria ya Tamko ya Sheria za
Kiislamu Sura ya 375 ili suala hilo litambuliwe
kisheria.
Endapo muswada huo ambao tayari
umechambuliwa na wadau ungepitishwa,
kungefanyika marekebisho kwenye kifungu cha
tatu baada ya maneno ‘all courts’ (Mahakama zote)
na kuongezwa maneno ‘including Kadhi
Courts’ (Ikijumuishwa na Mahakama ya Kadhi).
Hata hivyo, Jukwaa la Wakristo linaloundwa na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa
Makanisa ya Kipentekoste nchini (CPCT), lilisema
mapendekezo hayo “yanaibua mambo mazito ya
kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali na sheria hiyo itawaathiri hata wenye
imani tofauti.”
Msemaji Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania,
Sheikh Rajab Katimba akizungumza na
waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana.
Share this article :

Chapisha Maoni

 
Designed By AL HUDDAH
Islamic foundation
Copyright © 2013. RIAD BIN RUWEHY | All Rights Reserved