MUHTASARI
Sifa
zote njema ni zake Allah (Subhanahu wa Taala), Muumbaji wa vilivyo
dhahir na vilivyofichikana, Bwana wa Ulimwengu. Rehma na Amani ziwe juu
ya Habibul-Mustafa Muhammad (SwallaAllahu Alayhi wa Sallam)
ambaye ameletwa kwetu kuwa ni Rehma kwa ulimwengu. Nashuhudia kwamba
ameufikisha kwa ulimwengu ujumbe sahihi na muongozo wa haki kutoka kwa
Allah (Subhanahu wa Taala).
Makala hii imegawika sehemu nne. Sehemu ya kwanza ni utangulizi wa matumizi ya Sheria za Kiislamu
Tanzania
Bara. Sehemu ya pili inahusika na matumizi ya Sheria za Kiislamu kwenye
kipengele pekee cha ndoa za Kiislamu na masharti yake ili kusihi hiyo
ndoa. Pia namna ya hiyo ndoa ya Kiislamu inavyohitalifiana na sheria za Tanzania Bara. Sehemu ya tatu inajadili vipengele vyengine vya sheria za Tanzania
pamoja na uthibitisho wa kesi zilizowahi kutolewa maamuzi kwenye
masuala ya jamii ya Kiislamu. Sehemu ya nne na ya mwisho, inajumuishwa
kwa mawazo ya muandishi kuhusiana na namna ya Sheria ya Kiislamu
inavyonyongwa na lipi lifanyike ili kuokoa jamii ya Waislamu Tanzania Bara. Sehemu hii inapatikana mwisho kwa jina la hitimisho.
SEHEMU YA
KWANZA
UTANGULIZI
Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania
inajulikana wazi kuwa ni taifa lisilofungamana na dini, ni kwamba dini zote zina hadhi na nguvu sawa ndani ya Jamhuri ya Tanzania. Hivyo, Uislamu ni miongoni mwa dini kadhaa zilizomo Tanzania.
Tanzania
chini ya Katiba yake imetangaza uhuru wa mawazo au dhamiri, itikadi au
imani ikijumuisha uhuru wa kubadili dini au itikadi. Uhuru wa mtu
kuamini dini au imani atakayo umetawazwa chini ya Kifungu namba 19 cha
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania
ambacho kinaeleza kama ifuatavyo:
“(1)
Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, wa imani na wa uchaguzi
katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa kubadilisha dini au imani yake.
(2)
Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya
kutangaza dini, kufanya ibada na kuendeleza dini itakuwa huru na jambo
la hiari ya mtu binafsi; na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini
zitakuwa nje ya shughuli za Mamlaka ya Nchi.
(3)
Kila palipotajwa neno “dini” katika kifungu hiki ifahamike maana yake
ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au
kuambatana na neno
hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.”
Matokeo ya Kifungu hicho hapo juu ni kuwa Katiba ya
Tanzania
inaigawa dini kwenye mafungu mawili ambayo inazifanya dini zote ukiwemo Uislamu kuwa na hadhi tasa (negative status)
kwa kueleza kuwa Serikali haina mkono wake katika shughuli za dini.
Wajibu wa Serikali ni kuitetea haki hii inapotokezea uvunjwaji wake wa
kuabudu. Kwa upande mwengine, dini zote zinatambuliwa kuwa na hadhi
sanya (positive status) kutokana na kuwapatia wananchi haki ya
kuitangaza na kuimarisha maslahi ya dini ndani ya taifa lisilofungamana
na dini kwa kufuata sheria na kanuni za usawa.
Ingawa Kifungu cha 19 kinaifunga Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuingilia itikadi za dini, lakini
Tanzania
hii isofungamana na dini yoyote imetoa ruhusa ya kupitishwa sheria
zenye kuathiri imani na matendo ya wanaumini hasa wa Kiislamu. Kwani
Uislamu sio tu kuingia msikitini na kuswali; ni mwenendo mzima wa maisha
kuanzia kuzaliwa hadi kufa kwake. Uislamu ni mfumo kamili wa kuishi
unaozingatia mafundisho ya dini.
Tunashuhudia
Tanzania Bara kurithi baadhi ya sheria za Uingereza, kwa mfano Sheria
ya Usimamizi wa Mali zilizo Hafifu, sura ya 30 (The Administration of Small Estate chapter 30)
inayompa mzigo mzito maiti kurithiwa kwa Sheria za Kiislamu pale tu
atakapotangaza (kabla ya kufa) kwa mazungumzo au maandishi. Ikiwa
hakueleza nia ya kurithiwa kwa Sheria za Kiislamu basi atarithiwa kwa
sheria za nchi.
Matumizi
ya Sheria za Kiislamu Tanzania Bara zimetengwa kwenye mambo ya jamii tu
kama ndoa, talaka, mirathi na matunzo ya watoto. Sheria zilizorithiwa
kutoka kwa Muingereza ( kwa mfano Judicature of Application of Law Ordinance 1961-JALO na Tanganyika Order in Council)
zinaruhusu matumizi ya Sheria za Kiislamu kwenye vipengele vilivyotajwa
hapo juu. Pia Mahkama ya Mwanzo (Primary Court) ndizo zenye ruhusa ya
kusikiliza madai haya ya Waislamu[1].
Sheria ya Tanzania haijaweka kanuni ya Hakimu katika Mahkama ya Mwanzo
shurti ya kuwa Muislamu. Hivyo kwa sheria ya Tanzania madai ya wanandoa
wa Kiislamu yanaruhusiwa hata kusikilizwa na Hakimu asiyekuwa Muislamu
(Magistrate’s Courts Act of 1984).
Mpaka
hapa tu, utakuwa umetambuwa kuwa Tanzania Bara haina Mahkama maalum ya
kusikiliza madai ya Waislam kwa jina la “Mahkama ya Kadhi” ambapo
Mahkama hii ipo Kenya, Uganda na Zanzibar. Tanzania Bara wanatumia
Mahkama ya Mwanzo ambayo inatumika kusikilizia sio tu madai ya Waislamu
bali kwa makabila na itikadi nyengine zote. Pia Mahkama ya Mwanzo ina
uwezo wa kusikiliza kesi za madai na jinai kwa sheria za nchi.
Ni
ukweli usiofichika kuwa Mahkama ya mwanzo inawaathiri sana Waislamu
kwani haina Mahakimu wa Kiislamu wenye elimu ya Sheria za Kiislamu.
Tunatambuwa
pia kuwa Sheria za Kiislamu haitumiki katika nyanja zote za madai na
jinai kwa sababu Tanzania imejitawaza kuwa taifa lisilofungamana na
dini, hali ya kuwa bado Tanzania inaingilia uhuru wa kuabudu na kuzuia
Waislamu kufuata maamrisho ya Sheria za Kiislamu.
Mwaka
1971, matumizi ya Sheria za Kiislamu yalibanwa rasmi kwenye masuala ya
ndoa, talaka na mahari. Ili kuwa na nguvu kisheria juu ya masuala hayo,
ikapitishwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 (Law of Marriage Act 1971)
ambayo sio mahsusi tu kwa Waislamu bali kwa wananchi wote wa Tanzania
bila ya kujali tofauti za dini au imani. Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971
(SNM 1971) inazingatia masuala ya ndoa, talaka na mahari kwa muongozo wa
taratibu na ushahidi uliokuwa ukitumika zama za Muingereza. SNM 1971
inaweka uwiano wa kisheria kwenye masuala ya ndoa na talaka. Pia sheria
hii inatumika sawa sawa kwa Waislamu wote bila ya kujali madhehebu,
imani au jinsia.
SEHEMU YA PILI
KANUNI ZA NDOA YA KIISLAMU
Sheria
ya Ndoa ya Mwaka 1971 (SNM 1971) kwa uwazi kabisa inatangaza kuzitambua
ndoa za Waislamu na zile za wake zaidi ya mmoja. SNM 1971 haikufafanua
taratibu sahihi za Kiislamu za kuikamilisha hiyo ndoa. Mfano mahari,
akdi, posa n. k.
Kuna
mgongano wa umri wa mtu kuoa baina ya SNM 1971 na Sheria ya Kiislamu
kwani SNM 1971 inatangaza kuwa umri wa kuoa ni miaka 18 na kuolewa ni
miaka 15. Kwa taratibu za Kiislamu, mtoto wa kike/kiume akishafikia
balegh tu anaweza kuingia kwenye ndoa. Hii ina maana ya kusema kuwa
msichana akianza kutokwa na damu ya hedhi akiwa na umri wa miaka 12
hawezi kuolewa kwa vipengele vya SNM 1971 ingawa kwa Sheria ya Kiislamu
anaruhusika.
Kitu
chengine muhimu kwa ndoa kutambulika chini ya SNM 1971 ni kuwepo cheti
cha ndoa kama ni ushahidi wa ndoa. Cheti hicho cha ndoa ni lazima kiwe
kimesainiwa na kadhi, wanandoa na mashahidi wawili. Ingawa kwa Sheria ya
Kiislamu cheti cha ndoa au hata cha talaka sio lazima mpaka kufikia
kiwango cha kutoitambua ndoa kama isemavyo SNM 1971.
SEHEMU YA TATU.
Katika sehemu hii, tutajadili namna Sheria ya Kiislamu inavyotumiwa Tanzania Bara kwenye vipengele vifuatavyo:
1-TALAKA
Pale
ambapo SNM 1971 imetoa maelezo kuhusu ndoa na talaka, Sheria ya
Kiislamu haitotumika. Matokeo yake SNM 1971 imeweka sababu maalum za
kuitoa talaka na kuifanya ile kauli ya “talaka” kukosa nguvu ya kuivunja
ndoa. SNM 1971 inaweka njia mbili za kuivunja ndoa ambazo ni kifo na
amri ya Mahkama. Pia ili talaka ipatikane kutoka Mahkama kwa hao
wanandoa wa Kiislamu, ni lazima sharti tatu muhimu zitimizwe kabla ya
hao wanandoa kuomba hiyo talaka. Kifungu namba 107 (2) cha SNM 1971
kinaeleza:
1- Pande zote mbili wawe wamefunga ndoa kwa taratibu za Kiislamu.
2-
Wanandoa hao wamefikisha bila ya mafanikio ya kupatikana suluhu kwenye
Baraza la kusuluhisha ndoa na baraza hilo liwe limeshindwa kusuluhisha.
3- Pande yoyote iwe imefanya ‘jambo’ au ‘kitu’ kinachoweza kuivunja ndoa.
Katika kesi ya Rattansi Vs Rattansi[2]
wanandoa walitimiza masharti mawili ya mwanzo, nayo ni (a) wamefunga
ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu na (b) wameshindwa kupata suluhu
mbele ya Baraza la kusuluhisha ndoa. Lakini hamna yeyote kati ya
wanandoa hawa aliyefanya jambo au kitu kinachoweza kuivunja ndoa. Kwa
mujibu wa SNM 1971 inatambua uzinzi, matatizo ya unyumba, maradhi,
uwenda wazimu, ukatili, kifungo cha jela kuwa ni mambo yanayoweza
kuivunja ndoa. Lakini lile tamko la ‘talaka’ sio shurti na kwa njia
yoyote haiwezi kuivunja ndoa.
Kwenye kesi nyengine ya Abdallah Saidi Vs Manamkuu Yussuf[3]
ambapo mume alitamka talaka tatu wakati mmoja kabla ya kufika kwenye
Baraza la kusuluhisha ndoa. Kaimu Jaji Samatta alieleza kuwa Mahkama ina
nguvu ya kutoa talaka pale ambapo inapokubalika kuwa ndoa imevunjika
(kama uzinzi, matatizo ya unyumba n. k)
Hivyo, chini ya SNM 1971 ‘talaka’ haitambuliwi kuwa ni ‘kitu’ au ‘jambo’ ki/linachovunja ndoa.
Zipo
baadhi ya sababu za kuitoa talaka zinazoingiliana chini ya SNM 1971 na
Sheria ya Kiislamu. Lakini ushahidi wake unagongana na ule ulioelezwa
kwa Sheria ya Kiislamu. “Khula” ni miongoni mwa hizo, ambapo mke
anamlipa mume kupatiwa talaka. SNM 1971 haitambui “Khula” kama
ilivyohukumiwa kwenye kesi ya Aisha Chambala Vs Muhamadi Nyaseba[4] ambapo
mke alifungua kesi ya kuomba talaka kwa hoja ya yeye mke kushindwa
kuishi na mumewe kutokana na kukosekana matunzo. Mahkama haikuyapa nguvu
yoyote hoja hiyo kwani katika kesi hii hakuna ‘jambo’ au ‘kitu’
kinachoweza kuivunja ndoa hiyo. Kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu, mke
anaweza kujiengua katika ndoa ikiwa ni kwa mapenzi ya mke kuomba talaka
kwa shurti ya kurejesha mahari aliyopewa.
Jambo
la kushtuwa kwa Mahkama hizi kuwa hazitumii ushahidi wowote bali
kujipweteka kwa kujitosheleza na sababu tatu (Kifungu 107 (2) SNM 1971).
Juu ya hivyo, inaonesha wazi kuwa Mahkama hazitaki kufuata matakwa ya
Waislamu. Kwani zinapotimizwa shurti hizo, Mahkama hizi hizi hudai
kukimbilia ushahidi.
Katika kesi ya Ashura Salim Vs Ali Said[5]
ambapo mke alifungua madai ya talaka kutokana na ukatili, lakini
Mahkama ya Mwanzo ilikataa kutoa talaka kwa hoja ya kukosekana ushahidi.
Kwenye kesi ya Halima Athumani Vs Maulidi Hamisi[6]
mkata rufaa (Bi Halima) alifungua madai ya talaka kwa hoja ya ukatili
kutoka kwa mumewe. Hoja ya msingi iliyowekwa na Mahkama ni kuwa upo
uhalali wa Baraza lisilo la Kiislamu kusuluhisha ndoa na kukataa
kuwapatia talaka wanandoa wa Kiislamu? Kwani Mahkama ya Wilaya ilikataa
kuwapatia talaka kwa hoja hiyo juu. Uamuzi huu wa Mahkama ya Wilaya
ulipingwa na Mahkama Kuu kwani ‘sababu tu’ ya Baraza kutokuwa la
Kiislamu haiwezi kulifanya Baraza kuwa batili.
Kwa
maoni ya Mheshimiwa Jaji kuwa mke anaweza kufungua madai ya talaka kwa
njia ya ‘khul’ na mume anaweza akatumia ‘talaqa’ kufungua madai ya
talaka. Kwani kwa maelezo ya Mheshimiwa Jaji, Waislamu hawaendi
Mahkamani kuomba kupatiwa talaka ila wanaenda kupatiwa maombi ya
kusajiliwa hiyo talaka yao. Maoni ya Mheshimiwa Jaji ni sahihi lakini
kwa mujibu wa SNM 1971 kifungu 107 (1) na (2) ‘khul’ wala ‘talaqa’
hazina nguvu yoyote.
2-MATUNZO YA WATOTO.
SNM
1971 chini ya kifungu namba 123 inaipa nguvu kwa upande fulani hoja ya
Kiislamu kuwa mtoto (wa kiume/kike) aliye chini ya umri wa miaka 7 awe
kwa mama. Kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu mtoto wa kiume aliyetimiza
umri wa miaka 7 anaweza kuishi kwa baba na mtoto wa kike hana ruhusa ya
kuondoka chini ya mikono ya mama hadi aingie balegh.
Kuna hatua nne zilizoelezwa ndani ya SNM 1971 ambazo lazima ziangaliwe ili kutoa matunzo ya mtoto ama kwa baba au mama:
i- Usitawi wa mtoto (mfano mali, mazingira, elimu, malezi n. k)
ii- Maelezo ya wazee.
iii- Maelezo ya mtoto yataangaliwa ikiwa anaweza kujieleza.
iv- Sheria za mila na utamaduni.
Hivyo, usitawi wa mtoto unapewa kipaumbele kama ilivyotolewa hukumu kwenye kesi ya Zainab Pothoo[7] ambapo
iliamuliwa kuwa hamna mtu yeyote mwenye haki zozote dhidi ya mtoto.
Kinachoangaliwa zaidi ni usitawi wa mtoto na wala sio Sheria ya
Kiislamu. Kwa mujibu wa hukumu hii, ikiwa Mahakama zote zitaangalia tu
usitawi wa mtoto basi upo uwezekano wa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa
kukosa malezi ya mama mzazi au mtoto kupatiwa matunzo na mzee
(baba/mama) aliyekuwa si muislamu. Ilimuradi tu kuna maslahi ya fedha
kwa mmoja wa hao wazee, haingaliwi dini wala Sheria ya Kiislamu. Pia
inaweza kumfanya baba mzazi kutengwa na mwanawe halali na kupatiwa mama
wa kambo. Matokeo yake kwenye kesi ya Asya Amir Vs Ahmed David[8] mtoto
alizaliwa nje ya ndoa baadaye wazee wakafunga ndoa. Mahkama Kuu
ikajilazimisha kumtambua mtoto amezaliwa ndani ya ndoa na hivyo ni mtoto
halali. Akapatiwa mume matunzo ya mtoto ambapo kwa mujibu wa Sheria ya
Kiislamu ni kosa kwani ni mama pekee mwenye matunzo ya mwana aliye
haramu.
Katika kesi nyengine ya Saada Muyoyo Vs Hussein Ally[9]
baba mtu alikuwa sio baba halisi wa mtoto Khamisa lakini akafungua
madai ya matunzo ya wote kwa mtoto Khamisa na mtoto Pili. Mahkama ya
Mwanzo ilimpa matunzo kwa Pili na Khamisa. Lakini Mahkama Kuu ikaeleza
kuwa kwa vile ustawi wa mtoto unaangaliwa zaidi, na kwa vile watoto hao
wa kike wapo kwenye umri wa utoto ni bora wawe kwa mama hadi kufikia
umri wa kwenda shule. Kosa lililopo kwenye uamuzi huu (ingawa baba mzazi
aliomba hilo, lakini ombi lililokuwa batili haliwezi kukubaliwa) ni
baba kutozwa nguvu kutoa malipo kwa ajili ya matunzo ya watoto wote
wawili, hata kwa Khamisa ambaye si mwanawe halisi.
3. 1 MIRATHI
Sheria
za Tanzania Bara hazielezi ni sheria gani itumike pale ambapo marehemu
alifuata mila pamoja na Sheria ya Kiislamu. Lakini nguvu zaidi
inapelekwa kutumika sheria za kikabila kuliko sheria ya Kiislamu.
Sheria
ya Usimamizi wa Mali zilizo Hafifu (The Administration of Small Estate
Ordinance) inaamrisha kuwa masuala ya mirathi kwa pande zote mbili
ambazo ni waislamu, itumike Sheria ya Kiislamu. Lakini Sheria ya
Usimamizi wa Mali zilizo Hafifu haielezi namna ya kuigawanya hiyo mali
ya mirathi. Kwa mujibu wa Uislamu, kuna sheria maalum ya mirathi
inayotoka moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu (Qurani)[10]
ambayo ndio msingi mkuu wa Sheria ya Kiislamu. Hivyo sheria na kanuni
za mirathi kwa waislamu zipo na hatuna haja wala hapana uwezo kwa yeyote
kuwatengenezea Waislamu sheria zilizokuwa nje ya maamrisho ya Muumba.
Chini
ya Uislamu, mirathi inakwenda moja kwa moja kwa warithi chini ya
utaratibu uliopangwa. Haijapewa nguvu Mahkama isokuwa ya Kiislamu
kugawanya mali hiyo. Sheria ya Usimamizi ya Mali zilizo Hafifu (The
Administration of Small Estate Ordinance) inatambuwa kuigawanya mali kwa
njia za Kiislamu pale tu ambapo Marehemu ameeleza kwa maneno au
maandishi kurithiwa kwa taratibu za Kiislamu. Sheria ya Kiislamu
zinaeleza kuwa ni thuluthi 1/3 tu ya mali anayoweza kuiandikia wasia[11]. Hivyo, 2/3 inatakiwa iwe kwa warithi, mgao au zawadi ya mali kwa yeyote nje ya sheria ya mirathi isizidi thuluthi.
Masuala
ya jamii ya Waislamu nchini Tanzania yamefanywa kuwa na uhusiano wa
sheria za nchi na sio Quran au Sunnah. Vivyo hivyo kwa Mahkama kufuata
sheria za nchi tu. Matokeo yake, hata wasia ukitolewa mbele ya Mahkama,
utahukumiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi. Ikumbukwe kwamba
Katiba hiyo hiyo inakaa kuingilia masuala ya dini.
Wakati
huo huo, Sheria ya Kiislamu zinakataa kuandikia wasia kwa mtu yeyote.
Mfano wasia kwa asokuwa Muislamu au kwa atayakayemrithi n. k. Anaweza
kwa mapenzi yake Marehemu kutoa mali yake kama zawadi lakini kwa kiwango
kisichozidi thuluthi (1/3) ya mali yake. Matumizi
ya Sheria ya Kiislamu kwenye Mahkama za Tanzania unaonesha wazi
kuingilia kanuni za Sheria ya Kiislamu. Kwenye kesi ya Anwar Z. Mohammed Vs Saidi Selemani Masuka[12] ambapo Mahkama ya Rufaa ilitumia Ijtihad[13].
Hata wakili wa Mkataa Rufaa Muheshimiwa Korosso alishauri Mahkama
kutoitambua Sheria ya Kiislamu kwani inakwenda kinyume na Katiba
inayoeleza kuwa mtu yeyote ana haki ya kumiliki na kugawa mali (wasia
zaidi ya thuluthi) kwa namna apendavyo.
Katika
kesi hiyo ya Anwar dhidi ya Saidi, marehemu alikuwa ni mwanamke
aliyeolewa na Bw. Saidi. Marehemu aliandika wasia wa mali yake yote kwa
mumewe Bw. Saidi akimwacha mwanawe wa kumzaa ndugu Anwar bila ya urithi
wowote.
Ndugu
Anwar alikuwa mtoto wa Marehemu lakini kwa mume mwengine. Tutambue
kuwa, wasia zaidi ya thuluthi ndani ya Uislamu ni fasikh.
Kutokana
na wasia huo, Anwar hakuweza kumrithi mama yake kinyume na mafundisho
ya Sheria ya Kiislamu kwani Anwar anaweza kumrithi mama yake hata bila
ya wasia. Mahkama za chini zote zilimkatalia Anwar haki ya kurithi.
Mwishowe, Mahkama ya Rufaa kupitia kwa Mheshimiwa Ramadhani, J. A
ikatengua uamuzi wa Mahkama Kuu na kumruhusu Anwar kurithi. Hivyo
matumizi ya sheria za Tanzania na matumizi ya haki za lazima ‘fundamental rights’ bado yanahitaji kufafanuliwa barabara katika kutunga sheria zisizofungamana na dini.
3. 2 MIRATHI KWA WASOKUWA WAISLAMU.
Kabla
ya kuchambua kipengele hichi, ieleweke kuwa Uislamu umeweka vizingiti
na kuruhusu yenye manufaa kwa binaadamu wenyewe. Sheria ya Kiislamu
haina lengo la kumnufaisha jasho, damu, nguvu n. k. ya Muislamu
istarehewe na kudhalilishwa mbele ya wasokuwa waislamu. Hivyo Sheria ya
Kiislamu imeweka kizuizi kwa asokuwa Muislamu kumrithi Muislamu ili
kuupa nguvu Uislamu kwa kuiachia mali iendelee kwa kizazi kilicho cha
Kiislamu. Sheria ya Kiislamu inaeleza kuwa itakapotokezea mrithi kuwa si
Muislamu hataruhusika kumrithi Marehemu hata akiwa ni ndugu wa karibu.
Lengo kuu la kuweka kizuizi hichi ni kuimarisha dola/jamii ya Kiislamu.
Uamuzi
wa Mahkama za Tanzania unaonesha kuwa mahusiano baina ya warithi na
marehemu yanaangaliwa zaidi kwenye ndoa na uzazi. Hivyo, sifa ya mrithi
kuwa ni Muislamu iliondolewa kama ilivyohukumiwa katika kesi ya Shambaa Juma na wengine Vs Rashid Juma[14]
Maelezo ya kesi hii ni kwamba ikiwa dini itatumika kuwa ni kigezo cha
mirathi, hata asohusika (alimuradi ni Muislamu tu) anaweza kudai mirathi
kwa hoja ya dini. Kwa ufafanuzi ni kuwa Uislamu unatambua kuwa waumini
wote ni ndugu, lakini udugu unaozungumzwa hapa sio ule wa kurithi. Kwa
hivyo sio hoja ya dini pekee kuruhusu Muislamu kumrithi Muislamu
mwenziwe. Bali ni lazima uwepo pia uhusiano wa damu au ndoa. Ni wazi
kuwa Uislamu umekataza mirathi ya Muislamu ambaye amebadili dini au yule
alokuwa na uwezo wa kumrithi (kwa mfano mke, ndugu, baba n. k) lakini
akawa nje ya Uislamu. Hawa ndio makusudio ya Sheria ya Kiislamu. Hivyo,
hukumu hiyo ni mbaya kwa Waislamu kwani kigezo cha dini kwa Uislamu
kinaangaliwa sawa sawa na kigezo kuhusu chanzo cha uzazi na ndoa.
Msingi wa haki ya mirathi haukumalizia hapo kwenye kesi hiyo bali hata kwenye kesi ya Re Salum Omar Mkeremi[15]
ambapo mjane asokuwa Muislamu aliruhusiwa kumrithi mumewe alimuradi tu
ilikuwapo ndoa. Kwa Sheria ya Kiislamu, ndoa baina ya mke wa Kiislamu na
mume asokuwa Muislamu haikubaliki. Pia mhusika asokuwa Muislamu hawezi
kumrithi Muislamu kwa namna yoyote itakayokuwa.
Kwenye kesi nyengine ya Jumanne Selemani Vs Catherine Sindano[16]
mjane asokuwa Muislamu na asokuwa na mtoto alipewa nusu ya mirathi
wakati Sheria ya Kiislamu inaeleza kuwa mjane asokuwa na mtoto anarithi ¼
ya mirathi haikutumika. Kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu, bi Catherine
si Muislamu na hivyo haruhusiki kumrithi Muislamu kwa namna yoyote. Ni
kusema kuwa Mahkama za Tanzania zinafuata matakwa ya kuibeza Sheria ya
Kiislamu sio kuisimamisha.
3. 3 HAKI ZA WAJANE WA KIISLAMU KATIKA MIRATHI.
Nguzo ya haki na usawa kwenye jinsia imedhaminiwa ndani ya Katiba kifungu namba 12 inayozungumza kama ifuatavyo:
“(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wo wote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
(2) Hakuna sheria itakayokuwa na kifungu chochote ambacho ni cha ubaguzi wa moja kwa moja au kwa taathira yake.
(3)
Haki za raia, wajibu wa maslahi ya kila mtu yatalindwa na kuamuliwa na
mahakama pamoja na vyombo vya nchi na vinginevyo vilivyowekwa na
sheria.”
Dunia
imejikubalisha kuelewa kuwa Qurani inamnyima mwanamke mirathi sawa ya
ile ya mwanamume na hivyo kuonekana kuwa Qurani ina ubaguzi (AstaghfiruAllah).
Ni wazi kabisa kifungu hichi cha Katiba kinateka nyara Sheria za
Muislamu wa kike kurithi nusu ya kile anachorithi ndugu yake wa kiume.
Sheria za Kiislamu pia zinabezwa kwa kumpa mjane asokuwa na mtoto ¼ ya
urithi wa mume na 1/8 akiwa na watoto.
Kidogo
tu nichambue hapa kuwa mwanamke ndani ya Uislamu hajazuiliwa kupatiwa
zawadi ya mali ila ameshurutishwa mwanamme kumpatia makazi, kivazi,
chakula kwa mujibu wa sheria. Mahari anatoa mume kumpa mke hata iwe ni
dola milioni moja na bado vyote hivi vinakuwa kwa mke mali yake
isogawanywa na mume. Ingawa mume cha kwake ni nusu bin nusu kwa mke.
Dunia
inangalia kipengele cha mirathi tu ndani ya Uislamu kuwa na ubaguzi!
Wanawake mpaka wa Kiislamu waliokosa elimu na ufahamu sahihi wanafuata
mdundiko wa Magharibi bila ya kutafuta ukweli. Kama wanawake ni wenye
akili wadai wanaume kufuata hiyo Sheria ya Kiislamu. Kwani Uislamu
unamuamrisha mume kukaa na mke sio kumtelekeza, kumpa mahari sio
kumlaghai, kumpa matunzo sio kumuuza. Wallahi naapa kwa Yule Anayemiliki
nafsi yangu, hamna matunzo bora na ya ufakhari kwa mwanamke zaidi ya
Sheria za Kiislamu. Kama hazifuatwi hizo Sheria, ni wajibu mwanamke
kuzipigania na sio kuzipinga. Aidha kama dola zinataka haki basi siteo
nguvu kutekeleza sheria ya Kiislamu, angalau hizi za familia na mirathi.
Juu
ya hayo, Mahkama ya Tanzania Bara zinatumia mila na Sheria ya Kiislamu
kutambua haki za mirathi. Kwa upande mwengine wa kesi ya ReSalum, hoja kuu kwenye kesi hii ni sheria gani itumike baina ya Sheria ya Kiislamu au sheria za kikabila za Wahehe.
Mwisho,
Sheria ya Kiislamu ikachukua mkondo wake kwa marehemu kurithiwa kwa
mujibu wa Sheria ya Kiislamu. Lakini tuelewe kuwa ilikuwa ni hatua ya
upendeleo kwani kwa Kabila la Wahehe, mjane angeweza kuzuiwa haki ya
kurithi mali. Kwa maana hiyo Uislamu ndiyo wenye kutoa haki kwa
wanawake.
Hivyo,
daima Mahkama zinaangalia manufaa na sio kusimamisha Sheria ya Kiislamu
kama Quran na Sunnah inavyofafanua. Panapoonekana kufuatwa hiyo Sheria
ya Kiislamu basi kuna uwezekano mkubwa wa kumpendelea mwanamke au
inatumika pale kwa maslahi ya fulani tu.
Kwa
wakati tulio nao sasa, Mahkama ziweweka alama za kuangalia kwa kesi
ambazo zina mgongano wa sheria. Nazo ni; ikitokezea kuwa na mzozo wa
madai juu ya mirathi ya Muislamu ambaye pia akifuata mila za kabila
analotokea. Katika hili Mahakama inaweza kufuata alama zifuatazo:
1- Desturi ya maisha: Inaangalia namna marehemu alivyokuwa akiishi ndani ya jamii ambayo inafuata kanuni za kabila husika.
2- Nia ya marehemu: Mazungumzo na wasia unatazamwa ili kuonesha azma yake kutumika kanuni za Sheria ya Kiislamu au kabila.
4-KUITANGULIZA NDOA
Hii
ni aina ya ndoa zinazobarikiwa ndani ya Tanzania. Watu wanaoishi
kinyumba na kupata watoto bila ya kufunga ndoa rasmi wakiwa wamedumu
katika maingiliano hayo kwa muda wa zaidi ya miaka miwili basi
hutafsiriwa ni ndoa. Kifungu namba 160 SNM 1971 kinatangaza kuwa
mwanamke anayekaa kinyumba na mwanamme kwa muda wa zaidi ya miaka miwili
wanatambuliwa kuwa na hadhi ya ndoa, pia watoto waliozaliwa au
watakaozaliwa watatambuliwa kuwa ni wa ndani ya ndoa na hivyo ni halali.
Ndoa
zina nguvu na shurti maalum ndani ya Uislamu. Ikiwa wahusika watakaa
kinyumba na kuishi pamoja na kupata watoto bila ya kufunga ndoa ya
Kisheria za Kiislamu kwa miaka yoyote watakayokaa kinyumba ni kwenda
kinyume na maamrisho ya dini, hiyo ni haramu na wanatenda dhambi kubwa
yenye hukumu iliyosawa na uzinifu.
Ni
kosa kubwa kuitafsiri kwa uwongo Sheria ya Kiislamu kutoka kwa Majaji
kadhaa wa Tanzania Bara na kutangaza kuwa madhehebu takriban yote ya
Uislamu yanaikubali dhana ya kuitanguliza ndoa. Waislamu wanafuata
mwendo huu batili hawana hoja ya Kiislam, hawa ni waasi. Wanachofanya ni
kuingiza sheria za mila ndani ya Uislamu. Sheria za Kiislamu hazihitaji
nyongeza kutoka kwetu.
Hukumu hii imetolewa kwenye kesi ya Habibu Rahman Chowdhury[17]
Mheshimiwa Bw. Peter alieleza kuwa Uislamu unaruhusu kuidhinisha na
kuikubali ndoa kuwa halali katika mazingira ambayo hakukuwepo sherehe ya
arusi lakini ushahidi kuonesha kuwa wahusika walikusudia kufunga ndoa
na kuishi katika ndoa.
Hivyo,
kwa maoni ya Jaji Peter, hakuna haja ya kuitangaza/kuisherehekea arusi
bali nia ndio inayoangaliwa. Kinyume na mafundisho ya Uislamu ambapo nia
tu kwenye ndoa haikubaliki bali itangazwe na kushuhudiwa kwa mujibu wa
shurti za dini ya Kiislamu.
Katika kesi nyengine ya Pazi Vs Khamis[18] Jaji mhusika alitumia baraka za kesi ya Chowdhury. Hivyo maisha ya kinyumba pekee yalikubalika kuwa ni ndoa.
Suala
la kujiuliza, ni nani alijua nia ya hao watu kama kuoana? Kwanini mtu
aingie kwenye gharibu wakati jambo la dhahiri lipo? Ndoa ina sheria
zake, maadam hazikusimama kuifunga ndoa, basi hapo hapana ndoa. Ndoa ni
aina ya mkataba ambao umewekewa sheria maalum. Bila ya kufunga huo
mkataba na kufuata taratibu za sheria basi hamna ndoa.
5- KUUKANA UISLAMU (kurtadi)
Kwenye
sehemu hii, hatutazungumzia tu kuhusu kubadili dini ya Uislamu kwa
kuingia dini nyengine (kurtadi), bali tutajadili athari ya kurtadi
katika kipengele cha kuhodhi (kumiliki) mali.
Uislamu
una msimamo kuwa imani yake ya dini ndio sahihi na imani ilokuwa nje ya
mwenendo wa Uislamu kwa maamrisho ya Quran na Sunnah sio sahihi na
haukubaliki kwa maisha ya mwanaadamu yoyote.
Hivyo,
Muislamu yeyote atakayebadili mwenendo sahihi na kuanza kuupiga vita
Uislamu na Waislamu kwa kejeli, dharau na propaganda n. k (Mfano mzuri
rudia kadhia ya Salman Rushdi) basi huyo amefanya kosa la jinai na
adhabu itakuwa juu yake kwani ataleta chuki na fitna kubwa katika jamii
ya Uislamu.
Kwa sheria za Tanzania, mtu akitoka kwenye ukafiri na kuingia katika Uislamu, Sheria za Kiislamu hazitumiki juu yake.
Katika kesi ya Mtoro bin Mwamba Vs A. G [19] iliamuliwa kuwa Mkabila atakayebadili kuingia kwenye Uislamu hana haki ya kuhukumiwa kwa kutumia Sheria za Kiislamu.
Miongoni
mwa sababu za kutoa talaka ndani ya Sheria ya Kiislamu ni kurtadi,
vivyo hivyo kwa SNM 1971. Ajabu kuwa kipengele hichi cha kurtadi
hakitumiki kuzuia mirathi.
6- UGAWAJI WA MALI
Mali
za ndoa tunazojadili hapa ni zile baada ya kutolewa talaka. SNM 1971
inaeleza njia mbili muhimu zitumike kwa Mahakama kuigawa mali hiyo. Nazo
ni:
i) Mali iwe ni nguvu sawa ya wanandoa (wote wawili).
ii) Mahakama iigawe sawa kwa wanandoa.
Hivyo,
Mahakama itaangalia nguvu za mke na mume kwa kuigawanya mali sawa sawa.
Utata mkubwa uliokuwapo hapa ni kuhusiana na nini kinachojumuisha
kusemwa ‘nguvu sawa’ ambapo yalitafsiriwa katika kesi maarufu ya Bi Hawa Mohammed Vs Ally Sefu[20] uamuzi
katika kesi hii ni kuwa kazi za ndani ya nyumba anazofanya mke
zinamnasabu wa ‘nguvu sawa’ na zinachangia katika mali ya ndoa.
Kabla ya kuendelea mbele, kuna sababu za kutoigawa mali sawa sawa. SNM 1971 inaeleza:
(a) Mila za wahusika zinaizuia Mahakama kuigawa mali kwa mujibu wa sheria za nchi. AU
(b) Ikiwa mali ya ndoa haikupatikana kwa nguvu sawa baina ya wahusika. AU
(c) Ikiwa baina ya mhusika anamdai mwenziwe fedha au mali yoyote yenye thamani. AU
(d) Ustawi wa watoto pia utaangalia na ikiwa upo uwezekano wa kutoigawa mali sawa sawa baina ya mama au baba mzazi wa mtoto.
Kesi
ya Bi Hawa inaangukia kizuizi (a) kwani kwa sheria ya Tanzania, Uislamu
unaangukia hapa na kupewa hadhi sawa ya sheria za makabila. Sheria ya
Kiislamu inazuia mjane wa talaka kugaiwa mali ya ndoa aliyochuma mume.
Hivyo, haiwezi Mahakama kuamua kuigawa mali ya ndoa sawa sawa kwa kigezo
cha kazi afanyazo mke ndani ya nyumba. Jee haitoshi mume kupewa mzigo
juu ya mke wa kumlisha, kumpa makaazi, kumvisha, kumpa matibabu na sio
mke tu. Jukumu hili linakuwa juu ya baba hata kwa watoto wake. Mahakama
inaweza isione hili, inaangalia mke na mali tu. Mali zake mke daima
zitabakia kuwa za mke na mume hatakiwi kuzigusa kwa Sheria ya Kiislamu.
Katika sheria za Kiislamu akichumacho mke kinabaki ndani ya mikono yake
wala hamna ruhusa ya kuigawa.
Cha
kushangaza SNM 1971 imeshurutisha mke mwenye uwezo kumtumikia mume kwa
mavazi, chakula n. k pale ambapo mume hana uwezo. Sasa kuna waume
walokimbilia Mahakamani kuidai haki hii? Ipo pambo tu kwa sababu achilia
mbali jamii ya Waislamu, Jamii zote zaelewa jukumu la kuitumikia maisha
ya ndoa ni juu ya mume.
Ni
ukweli usiofichika, Sheria ya Kiislamu inapigwa vita hata kwa vipengele
vidogo tena vilivyo sawa kwa imani nyengine. Waislamu wana wajibu wa
kuusimaimisha Uislamu kuanzia sheria ndogo mpaka kubwa. Kwani Qurani
unaamrisha Muislamu aingie kwenye Uislamu mzima mzima. Sio nusu anafata,
mengine kuyaacha. Mfano tu wa hijabu, Uislamu umeshurtisha wanawake
wote sio kwa WachaMungu wa kike tu kama wafanyavyo imani nyengine za
dini. Uislamu haumnufaishi mmoja na kumuacha mwengine.
Hoja ya talaka kuathiri mali za ndoa inajadiliwa vizuri katika kesi ya Bibie Maulidi Vs Mohamed Ibrahim[21] ambapo
wahusika walioana kwa Sheria ya Kiislamu na kuachana kwa tamko la
‘talaka’ na kubarikiwa (kuruhusiwa) talaka hii mbele ya uamuzi wa
Mahakama ya Mwanzo. Lakini kuhusu ugawaji wa mali ya ndoa, ikahitaji
kuangalia ushahidi wa ubia (mchango) baina ya mume na mke. Hoja ya
msingi katika kesi hii ilikuwa, jee upo uwezekano wa kazi za ndani ya
nyumba kuwa ni ubia? Mahkama ilijikubalisha kuwa mke amefanya mchango
katika mali ya ndoa na kutoa uamuzi wa kuigawanya sawa sawa. Katika
rufaa ya Mahkama Kuu ilitupilia mbali hoja ya kazi za nyumbani kuwa ni
mchango sawa kwani mke alipatiwa nyumba aliyojengewa kama ni zawadi
kutoka kwa mumewe yenye thamani ya Tsh 40,000/-
Uhakika
ni kuwa uamuzi huo wa Mahkama ya Mwanzo ulikwenda kinyume na taratibu
za Kiislamu ambapo Uislamu unatambuwa mali ya kila mhusika na zawadi
baada ya kuachana.
Pia,
mume alijenga nyumba hiyo kama ni zawadi na sio kwa lengo jengine. Ni
kusema kuwa Mahkama Kuu haikuigawa mali hiyo kwa hoja ya ‘nguvu sawa’ na
kuridhika Mahkama kwa nyumba aliyozawadiwa.
SEHEMU YA NNE
HITIMISHO
Kama
tulivyopitia mawazo tofauti ya Majaji na Sheria za Tanzania, tumetambua
kuwa Sheria ya Kiislamu inawekwa pamoja na Sheria za Makabila. Kawaida
ya makabila zina sheria kutokana na urithi na imani au itikadi. Tofauti
na Uislamu kutumia Qurani ambayo inazaidi ya miaka 1400 kuwa ndio Katiba
yao. Sasa Tanzania na Dunia kwa ujumla ituoneshe sheria yoyote
inayotumika hadi leo yenye zaidi ya miaka mia moja tu ambayo haikuwahi
kufanyiwa marekebisho yoyote. Ukweli kuwa hamna.
Uislamu
unasheria zake maalum, kuziweka sheria hizi pamoja na zile za makabila
ni kumfanya Mwenyezi Mungu na Kitabu Chake kuwa na hadhi ya miungu ya
kikabila.
Sababu
hii ya kuichanganya Quran na Sunnah (Shariah) pamoja na makabila ndio
chanzo cha kufanya Mahkama kujaribu (bila ya mafanikio) kuikosoa Sheria
ya Kiislamu. Yareti kama Tanzania Bara ingeliachia Waislamu kuhukumiana
kwa sheria zao. Mahkama za Tanzania zisingefikia hatua ya kuikosoa
Sheria ya Kiislamu kama tulivyoona katika kesi tulizojadili.
Juu ya tofauti kubwa baina ya Sheria ya Kiislamu na zile za makabila (baynal maghrib wal mashrik na bayna ssamaa’ wal ardh),
bado zinajumuishwa pamoja kwa sheria za Tanzania kama SNM 1971, Sheria
ya Usimamizi wa Mali Hafifu na Katiba yenyewe. Pia sheria za kurithi
kutoka utawala wa Muingereza zimeathiri matumizi ya Sheria ya Kiislamu
nchini Tanzania.
Ni
utambuzi wa wazi kuwa SNM 1971 inaitikia ule wimbo wa ‘Beijing’
kumpendelea mwanamke kwa madai ya haki na usawa kuimarisha na kukuza
haki za wanawake kuliko kutoa uamuzi kwa haki. Kama tunavyoona SNM 1971
inaweka usawa wa talaka baina ya mume na mke wakati Uislamu umempa
usimamizi wa talaka mwanamme. Hili ni jukumu kwa wanaume sio upendeleo.
Ndani ya Uislamu hakuna kigezo cha kusema Imamu (aliye juu) kuwa ni bora
kuliko maamuma. Wote ni sawa, ila kwenye jahazi lazima awepo kiongozi
kwani nahodha wawili hawakai pamoja. Ndivyo kwa Uislamu kumteua mwanamme
kuwa msimamizi wa masuala ya ndoa na ndio akapewa majukumu chungunzima
kuanzia kutoa mahari, kugharamia makazi na mengineyo. Jee hatuoni huu
mzigo alioubeba mume? Kama wa kusimama kutetea jinsia ndani ya Uislamu
ni wanaume lakini katu hawatasimama kutetea dhulma kwani wamekubali
jukumu hili kuwa lao.
Inaelekea
lengo la kupitisha sheria kama ya SNM 1971 ni kumpa nguvu mwanamke
iliyokuwa nje ya uwezo wake. Kwani kwa Tanzania kuiwekea sheria Uislamu
ni kuitoa kasoro dini hii. Hii ni dini kamili na ndio maana haieleweki
kwa wale wanaofuata dini au itikadi zenye kasoro chungu nzima. Hao
hawaelewi falsafa ya Uislamu hadi pale watakapoondoa taka taka nyoyoni
mwao. Nyoyo zilizojaa taka taka haziwezi kuiona haki.
Tumeshuhudia baadhi ya wanasheria wa Tanzania[22]
kueleza kuwa miongoni mwa malengo ya kupitisha SNM 1971 ni kuwawezesha
wanawake (haswa wa Kiislamu) kupatiwa talaka bila ya kutilia maanani
vizingiti vya Sheria ya Kiislamu.
Kama
tunavyotambua kuwa Mahkama za Kadhi zipo Afrika ya Mashariki yote
Kenya, Uganda na Zanzibar. Lakini bado mjadala wa Tanzania Bara kuwa na
Mahkama yake ya Kadhi haujatatuliwa, ijapokuwa Kadhi sio tamko
lililotakatifu kutoka Qurani Tukufu. Historia inaonesha kuwa ‘Kadhi’
ilianza kipindi cha utawala wa Ufalme wa Umayyad (Umayyad Dynasty) na
kazi zake zilikuwa ni kusimamisha haki na kutoa ufafanuzi kwenye
vipengele vya Sheria ya Kiislamu. Kadhi waliwajibika kutumia Quran na
Sunnah.
Ingawa
sasa zipo jitihada zinazoonekana kufanyika kuanzisha Mahkama ya Kadhi
Tanzania Bara, lakini huenda ikawa Mahkama ya Kadhi kuwa ni jina zuri
nje lakini isiyo na maslahi kwa Waislamu kama ilivyo ofisi ya Mufti kwa
Zanzibar. Hivyo, taratibu zifuatwe kuhakikisha Mahkama ya Kadhi itafanya
uadilifu na lengo kuu liwe kuwawezesha Waislamu kufuata muongozo wao
sahihi wa Quran na Sunnah kwa njia ya kusimamisha haki na kutoa
ufafunuzi kwenye vipengele vya Sheria ya Kiislamu.
Ieleweke
na itambulike kuwa Waislamu wa Tanzania kutia nguvu kuanzishwa Mahkama
ya Kadhi hauna lengo la kurudisha utawala wa Kiislam Tanzania Bara kwa
kuanzisha dola ya Kiislamu. Waislamu wanadhamiria kuzikuza imani
zilizokuwa hafifu na zinazokaribia kupotea kwa kuanzisha Mahkama maalum
kwa Waislamu ambayo itasimamia masuala ya jamii ya Waislamu akili na
waangalie mwenendo wa Mahakama ya Kadhi nchini Kenya, Uganda na
Zanzibar. Mahakama hizo hazijaleta mitafaruku wala kulaumiwa kutotenda
haki. Makosa ya kibinadamu hutokea, nayo hushughulikiwa kama taratibu za
kisheria zilivyo
MAREJEO:
KATIBA YA JAMHURI YA TANZANIA 1984.
SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971
ESSAYS ON LAW AND SOCIETY by Legal Aid Committee, Faculty of Law, University of Dar-es-Salaam. MWAKA
WOMAN IN ISLAM, B. Aisha Lemu and Fatima Heern, Islamic Council of Europe 1978.
THE SECULAR STATE AND THE STATE OF ISLAMIC LAW IN TANZANIA presented by Makaramba on 21st to 23rd of July 2000 at The Islamic Law in Africa Project (ILAP), University of Cape Town – South Africa.
THE STATUS AND APPLICATION OF ISLAMIC LAW IN TANZANIA by Robert V. Makaramba.
CUTOMARY LAW OF TANZANIA, James, R. W and Fimbo, G. M
Website:
[1] Kifungu cha 18 (1) cha Sheria za Mahkama za Hakimu (The Magistrate Courts Act of 1984)
[2] (1971) TLR no. 55
[3] (1978) LRT no. 43
[4] Rudia makala ya Makaramba
[5] DSM H. C (P. C) matr. Civ App No. 39 of 1973 (unreported)
[6] H. C (1991) TLR pg. 79
[7] (1959) EA pg. 917
[8] (1968) HCD namba 206
[9] (1971) HCD namba 9
[10] Suratun-Nnisaa: 11
[11]
Sayyidna Umar (RadhiyaAllahuAnhu) alitaka kuitowa ardhi yake yote kuwa
waqfu, lakini Mtume (SwallaAllahuAlayhi Wasalaam) alimzuia.
[12] Rudia makala ya Makaramba
[13]
Ijtihad ni maelezo binafsi ambayo yanafungamana kutoka Quran na Sunnah.
Ijtihaad inatumika na Ulamaa maalum wa Kiislamu anayeitwa Mujtahid.
Ijtihad imezuiwa kutumika karne ya 10 Hijriya. Hivyo, matumizi ya
Ijtihad hayakubaliki kwa Waislamu seuze kwa wasokuwa Waislamu
[14] (1966) C. A. D/80/1966 reported in James, R. W and fimbo, G. M CUSTOMARY LAW OF TANZANIA, E. A. L. A, 1973 pg 174-175.
[15] (1978) LRT namba 18
[16] Rudia makala ya Makaramba
[17] (1921) LR 481 A 11 4
[18] (1968) HCD no. 18
[19] (1953) TLR
[20] CA no. 9 of 1983
[21] HCT (1989) TLR pg. 162
[22] Mheshimiwa Katiti (Justice Katiti) “bunge halikukusudia kupitisha sheria hii mpya (SNM 1971) iwe ni ngumu kwa Waislamu wanawake kuomba talaka, kama vile ilivyokuwa kwa sheria za zamani.”
+ coment + 1 coment
Je naweza nikapatA nakala hii kwa lugha ya kiingereza
Chapisha Maoni