Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo.
Kundi la wakazi wa kijiji cha Nkome wilayani Geita,
Mkoa wa Geita, wameandamana kisha kutelekeza
maiti ya mwenzao, Mlangila Tigamanywa (22),
mbele ya kituo cha polisi cha Nkome wakidai
baadhi askari wake wamemuua kwa kipigo.
Mlangila anadaiwa kushambuliwa kwa kipigo na
askari hao muda mfupi baada ya baba yake mzazi,
Bigamanywa Mlangila, kumfikisha kituoni hapo
kwa tuhuma za kuvunja dirisha la nyumba yake.
Mbali na mwenyekiti wa kijiji cha Nkome kilichopo
Kata ya Bugando, Angelo Daniel, kuthibitisha
kutokea kwa kushambuliwa kwa kipigo hicho
usiku wa Desemba 19, mwaka jana, alisema
alipelekwa kituoni hapo akiwa na afya njema.
Alisema siku iliyofuata, aliamka akiwa hoi
kutokana na kinachodaiwa kupewa kipigo na
askari hao walioshirikiana na mgambo aliyekuwa
zamu kituoni hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo,
amethibitisha maiti ya Mlangila kutekelezwa
kwenye mbele ya kituo hicho na kuahidi
kufuatilia, kisha
kutoa taarifa kamili za tukio hilo.
Hata hivyo, Kamanda Konyo hakutaka
kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi, akisema
alikuwa akiekelea kwenye tukio la wachimbaji
kufukiwa na kifusi kwenye mgodi wa dhahabu
katika kijiji cha Nyarugusu.
Baadaye Kamanda huyo akizungumza na
NIPASHE, alisema Mlangila alipigana na mgambo
kwenye kituo hicho cha polisi ambaye inadaiwa
alikwenda kumkamata baada ya baba yake
kuripoti tuhuma dhidi yake.
Alisema hata hivyo alizidiwa nguvu na mgambo
huyo.
Kwa mujibu wa Konyo, mgambo huyo
anashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, kaka wa marehemu,
Galidi Lukanazya (35), alidai mdogo wake aliuawa
baada ya kupigwa na askari wawili wa kituo hicho
kwa virungu na mateke sehemu mbalimbali za
mwili wake. (Majina ya askari hao na mgambo
huyo kwa sasa tunayahifadhi).
Alidai kipigo kwa mdogo wake kilianza baada ya
kuondoka kwa mkuu wa kituo hicho, Gwaga
Mtawa, saa mbili za usiku kwenda kutazama
taarifa ya habari kwenye moja ya ukumbi uliopo
kijijini hapo.
“Sababu za baba kumpeleka kituoni hapo
ilitokana na kuvunja dirisha la nyumba...ni baada
ya kukuta baba akiwa ameweka mpangaji
kwenye chumba alichokuwa akilala
Mlangila...alipouliza sababu za kuingiza mpangaji
kwenye chumba hicho baba, alisema nyumba hiyo
ni mali yake...ndipo Mlangila akazunguka nyuma
ya nyumba na kuanza kuvunja dirisha,” alisema.
“Baada ya kuona hali imekuwa hivyo, baba
aliamua kutoa taarifa kituo cha polisi, askari
walifika kisha wakamkamata na kumpeleka
selo...lakini wakiwa njiani Mlangila alionekana
kulalamika kuwa anaonewa na ndipo wakaanza
kurushiana maneno hadharani,” alisema.
"Binafsi ninachokiamini waliamua kumtembezea
kipigo baada ya kuhisi amewadharau wakati
wakimpeleka kituoni...na walitambua kwa kuwa
wameshamfikisha mahali hapo wana uhuru wa
kufanya wanavyojisikia...ndipo wakamjeruhi na
baadaye kumpeleka kwenye zahanati ya Nkome
kabla ya kumhamishia kwenye kituo cha afya cha
Nzera na baadaye Hospitali ya Wilaya ya Geita.
Habari zinadai kuwa baada ya kipigo hicho,
Mlangila alizirai huku akitokwa damu puani na
masikio na ndipo askari hao waliposhtuka na
kuamua kumkimbiza zahanati ya kijiji hicho na hali
ilipoonyesha kuwa mbaya, alihamishiwa kwenye
kituo cha afya cha Nzera.
Desemba 24, mwaka jana alihamishiwa kwenye
Hospitali ya Wilaya ya Geita na Desemba 31
walimpeleka tena hospitali ya Misheni ya
Sengerema, mkoani Mwanza kwa matibabu zaidi.
Imedaiwa kuwa Januari 4, mwaka huu hali yake
iliendelea kuwa mbaya na ndipo walipomhamisha
tena na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Mwanza kabla ya kukumbwa na mauti
Januari 9, mwaka huu.
Baada ya maiti yake kuwasili jana nyumbani kwao
kwa maziko, baadhi ya ndugu jamaa na marafiki
walipinga kuendelea na huduma hiyo na kudai
yanapaswa kufanywa na polisi na mgambo
waliosababisha kifo chake.
Kutokana na hali hiyo, kundi wanakijiji hao,
walibeba maiti hiyo isha kuitelekeza mbele ya
kituo hicho wakiwa wameifunika sanda nyeupe
huku baba wa marehemu huyo akitiwa mbaroni
kwa tuhuma za kuhusika na kifo hicho.
Habari zilizopatikana wakati tunakwenda
mitamboni jana usiku, zilieleza kuwa Ofisa wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Geita, John
Maro, alikuwa kwenye eneo la tukio kuwasihi
ndugu na jamaa wa marehemu wakubali
kuchukua maiti kwa maziko huku jeshi hilo
likiendelea na hatua nyingine za kusheria.
CHANZO: NIPASHE
Chapisha Maoni