Tuwe Waislamu wakweli

0 coment

Tuwe Waislamu wakweli


INAJULIKANA kwamba mtu anakuwa Muislamu kwa kutamka Shahada ambayo ina maana pana sana lakini maneno yake ni machache tu:
La ailah illallah Muhammadur-Rasulullah.
"Hakuna Mungu isipokuwa Allah: Muhammad ni Mtume wa Allah".

Kwa kutamka maneno haya mtu hubadilika mabadiliko makubwa sana. Alikuwa kafiri sasa anakuwa Muislamu. Alikuwa si nadhifu na sasa amekuwa mtwaharifu.. Alikuwa anastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na sasa ni kipenzi cha Mungu. Alikuwa ni wa kwenda Jahannam, ssa milango ya pepo iwazi kwa ajili yake. Wala hayaishii hapa.

Tokana na Shahada mabadiliko makubwa humtokea kinyume na wengine. Wale wote waitamkao huungana pamoja kufanya umma mmoja, ambapo wale wanaokanusha, hufanya kundi jingine. Kama baba atatamka Shahada na mtoto hataitamka, baba si baba tena na mwana si mwana tena kwa mnasaba wa imani. Mwana hatarithi mali ya baba yake. Hata mama na dada itawabidi kujifunika shungi zao kwa sitiri mbele yake na kujitenga naye. (Japo sharia haimlazimishi mama au dada kujisitiri na kujitenga na mwana au kaka aliyekafiri, hata hivyo mama na dada walio na imani ya hali ya juu hufanya hivyo).

Kinyume chake mtoto aliyezaliwa katika familia ya Kiislamu lakini akaikana Shahada, hupoteza haki na uhusiano wote katika familia hiyo. Hii huonyesha kuwa Shahada ni jambo kubwa liwezalo kujenga uhusiano kati ya mtu ajinabi na mwingine, na ambalo pia laweza kukata uhusiano kati ya jamaa na jamaa. Uhusiano wa shahada ni wenye nguvu na ni bora zaidi kuliko uhusiano wa damu.

Kwanini tofauti kubwa namna hii?
Sasa fikirini kwa makini, sababu ya kuwepo tofauti kubwa kama hiyo kati ya binadamu na binadamu. Kuna nini hasa katika Shahada? Ni neno fupi tu lenye herufi chache. Je, Shahada ikitamkwa hufanya kazi kama uchawi na kusababisha hayo mabadiliko makubwa kwa anayetamka? Jambo dogo kama hilo, kweli linaweza kusababisha tofauti kubwa kama baina ya mbingu na ardhi kati ya binadamu na binadamu?

Kiwango kidogo tu cha akili kinatosha kuwadhihirishia kuwa kufunua mdomo na kuitamka tu hiyo Shahada hakuwezi kuleta athari kubwa kama hiyo. Wakristu wanaamini kuwa bila shaka kutamka tu "Utatu Mtakatifu" (Holy Trinity) kunampa mtu uokovu na uzima wa milele, japo hamna yeyote anayeuelewa wala anayeweza kuuelezea vilivyo huo "Utatu Mtakatifu!" Hii ni kwa sababu wao wanaamini kuwa mafanikio yako katika herufi. Ukitamkwa "Utatu Mtakatifu" milango ya miujiza imefunguliwa na uokovu ndio natija. Lakini si hivyo katika Uislamu. Hapa la muhimu ni maana. Athari ya maneno iko katika maana yake. 

Kama maneno hayana maana au hayazami akilini na hayaleti taathira katika imani na matendo, basi kuyatamka tu maneno ni mchezo, kujidanganya na kazi bure.
Kama ungekuwa unatetemeka kwa baridi kali, nawe ukaanza kupiga kelele, "blangeti, blangeti", kiwango cha baridi hakitakupunguka hata useme kucha neno blangeti mara milioni kwa tasbihi. Lakini mara tu utakapojifunika blangeti utasalimika na baridi. Au kama una kiu nawe ukaanza kusema siku nzima, 'maji, maji', kiu chako hakitakoma. 
Lakini ukinywa maji kiu yako itakatika. Au kwa upande mwingine, kama unaumwa kichwa na ukawa unasema tu, 'Aspro, Aspro' Kichwa hakitapona hadi utakapomeza Aspro ndipo utakapopona. Hivyo ndivyo ilivyo Shahada. Kuitamka tu hakuwezi kuleta mabadiliko makubwa ya kumbadilisha kafiri kuwa Muislamu, muovu kuwa mwema, aliyelaaniwa kuwa mpendwa au kiumbe duni kuwa mtukufu.

Mabadiliko hayo yanawezekana tu pale unapoelewa maana ya Shahada na kuifanya izame akilini mwako. Na utakapoyatamka kwa kuelewa maana yake halisi utambue jukumu kubwa unalobeba mbele ya Mungu na dunia nzima tokana na kukiri hiyo Shahada. Na baada ya kuelewa kinaganaga maana halisi ya kukiri yaliyomo ndani ya Shahada, lazima hiyo Shahada itawale maisha yako yote, kiasi ambacho lolote lililo dhidi ya majukumu ya Shahada wewe ulikane. Baada ya kuikiri Shahada, haupo huru kama walivyo washirikina ambao hufanya walitakalo. Wewe baada ya kufungika na Shahada, huna budi kufuata kila kinachoamrishwa na Shahada na kujizuia na kila kinachokatazwa na Shahada. Kama kuitamka na kuikiri Shahada kutafanyika kwa muundo huu, mtu atakuwa Muislamu wa kweli.
Share this article :

Chapisha Maoni

 
Designed By AL HUDDAH
Islamic foundation
Copyright © 2013. RIAD BIN RUWEHY | All Rights Reserved