Manesi
wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Morogoro wameingia kwenye kashfa
nzito ya kusababisha kifo baada ya kudaiwa
kumtumbukiza mtoto mchanga kwenye ndoo
kwa zaidi ya saa 3.
Tukio hilo ambalo kwa sasa ni gumzo mkoani
hapa lilijiri hivi karibuni ambapo mwanamke
aitwaye Zainabu lsmali, mkazi wa Kididimo jirani na
Chuo Kikuu Cha Kilimo Cha Sokoine ‘SUA’ alishikwa
na uchungu wa kujifungua na kukimbizwa katika
hospitali hiyo kwa msaada wa jirani yake
aliyejitambulisha kwa jina la Mama Sira Manga.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda juu ya tukio
hilo, Mama Manga alikuwa na haya ya kusema:
“Huu ni uzembe mkubwa wa manesi. Tulipofika
hospitali mtoto alizaliwa akiwa hai lakini alikuwa
njiti kwani alikaa tumboni kwa mama yake miezi 7
badala ya 9.
“Cha ajabu usiku huo manesi baada ya kumcheki
mtoto walisema ni wa kike lakini eti walidai
amekufa hivyo waliamua kuchukua matambara ya
mzazi yaliyotumika kujifungua na kumzoa mtoto
huyo na kumuweka kwenye ndoo ambayo kwa
kawaida sisi wazazi huwa tunakwenda nazo leba.
“Walituambia tukazike, unajua kutoka hospitali
hadi Kididimo juu ya Milima ya Uluguru ni mbali na
gari lilichelewa kutufuata hivyo mtoto huyo alikaa
kwenye ndoo zaidi ya saa 3.
“Tulipofika nyumbani na kumtoa mtoto kwenye
ndoo tukamuona anahema na kufumbua macho
baada ya kumtingisha akakohoa ndipo
tukamkimbiza tena hospitali.
Pamoja na jitihada za manesi hao, kesho yake
mtoto huyo alifariki dunia baada ya kitovu chake
kuingiza hewa kwani kilikuwa bado hakijakatwa.
Mama wa mtoto huyo, Zainabu alipotakiwa
kuzungumzia tukio hilo alisema:
“Roho inauma sana lakini mzungumzaji wa tukio
hilo ni mume wangu.”
Baba wa mtoto huyo, Haji Kondo alisema: “Ni kweli nimempoteza
mwanangu lakini nisingependa kutoa lawama
kwa manesi kwani mke wangu bado anaendelea
kuzaa.”
Mwandishi alifika hospitalini hapo na
kuzungumza na daktari mfawidhi, Dokta Rita
Lyamuya ambapo alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli tukio hilo limetokea kwenye wodi yetu
ya wazazi.
“Manesi walitimiza jukumu lao la kumhudumia
mzazi lakini kwa bahati mbaya tuna changamoto
ya umeme kukatika bila taarifa hivyo wakati
manesi wakimzalisha alijifungua mtoto njiti.
“Ghafla umeme ulikatika na kutokana na giza,
manesi walijua mtoto amekufa hivyo waliwaeleza
wanandugu kwamba mtoto amefariki dunia.
“Ndugu walimchukua walipofika kwao na kukitoa
kwenye ndoo walibaini mtoto bado yupo hai.
“Walimleta tena hapa hospitali na tulifanya juhudi
za kumtibu lakini kwa bahati mbaya amefariki
dunia.”
Chapisha Maoni