Wakati mjadala mkali ukitarajiwa kuibuka katika
Mkutano wa 18 wa Bunge unaoanza leo kuhusu
uanzishaji Mahakama ya Kadhi, Jukwaa la Wakristo
Tanzania limeitaka Serikali kuachana na muswada
huo ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa
inayopinga ubaguzi na kutofungamana na dini
yoyote.
Suala la kuanzisha Mahakama ya Kadhi limo katika
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki ijayo na
unalenga kufanya mabadiliko katika Sheria ya
Tamko ya Sheria za Kiislamu Sura ya 375 ili suala
hilo litambuliwe kisheria.
Endapo muswada huo ambao tayari
umechambuliwa na wadau utapitishwa, katika
sheria hiyo kutafanyika marekebisho kwenye
kifungu cha tatu baada ya maneno ‘all
courts’ (Mahakama zote) wataongeza maneno
‘including Kadhi Courts’ (Ikijumuishwa na
Mahakama ya Kadhi).
Hata hivyo, Jukwaa la Wakristo linaloundwa na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Umoja wa
Makanisa ya Kipentekoste nchini (CPCT) limesema
mapendekezo hayo “yanaibua mambo mazito ya
kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na
sheria hiyo itawaathiri hata wenye imani tofauti.”
Tamko la Jukwaa hilo lililokutana Januari 20
kujadili uanzishwaji wa mahakama hiyo ni mtihani
kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye Septemba
29, mwaka jana katika mkutano wa Bunge la
Katiba aliahidi kuliwasilisha suala hilo katika
mkutano wa Bunge unaoanza leo ili kuanza
mchakato wa uanzishwaji wa chombo hicho.
Pinda alitoa ahadi hiyo kuwapoza wajumbe wa
Bunge hilo kutokana na baadhi yao
kuhamasishana kuipigia kura ya kukataa Rasimu
ya Katiba, iwapo chombo hicho kisingeingizwa
katika Katiba.
Pinda aliahidi ifikapo Januari 2015, Sheria ya
Mahakimu, sura ya 11 na Sheria ya Kiislamu sura ya
375 zitafanyiwa marekebisho ili kutambua
Mahakama ya Kadhi kwa lengo la kuhakikisha
umoja na mshikamano vinadumu kwa Watanzania.
Wapingwa katika Kamati
Uanzishwaji wa mahakama hiyo pia uliibua
mvutano mkali katika vikao vya Kamati ya Bunge
ya Katiba, Sheria na Utawala wiki iliyopita na
wajumbe walisema uwezekano wa kuanzishwa
kwake ni mgumu.
Katika vikao hivyo, ilielezwa kuwa kati ya wadau
15 kutoka taasisi za dini, wanaharakati, wanasiasa,
wanasheria na wasomi waliofika mbele ya kamati
hiyo, ni mdau mmoja tu aliyekubali kuanzishwa
kwa mahakama hiyo.
Miongoni mwa wadau hao ni; Islamic Propagation
Centre (IPC), Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),
Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, CCT,
TEC, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.
Wengine ni Baraza la Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania (BMKT), Mwakilishi wa Kanisa la Wasabato
(SDA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jukwaa la
Katiba Tanzania (Jukata), Profesa Abdallah Safari na
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Chapisha Maoni