Dini
ya Kiislamu ni mwenendo ambao umekamilika usiotaka kuzidishwa mapambo
ukawa mbaya wala kupunguzwa ukawa pungufu. Ni kufuata maamrisho ya
Qur-aan na Sunnah ya Mtume Habiybul-Mustwaafa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam).
Kuna
mambo mengi sahihi ambayo Muislamu wa kweli anaweza kukithiri kuyafanya
bila ya kuyamaliza hadi kufikia hatima ya maisha yake. Kwa mfano aweza
kukithiri kwa funga za Sunnah, kisimamo cha usiku, kusema ukweli na
mengineyo mengi tu.
Kwa
wengine mambo hayo ni magumu na mazito kuyatenda. Ndipo hutafuta yale
mepesi na kuyafanya ndio ibada zao. Na bila ya shaka binaadamu wote sio
wavumbuzi, ni wachache wanaovumbua na wengine hufuata mkumbo tu.
Mayahudi na vibaraka vyao wameupamba ulimwengu kwa michezo ya mpira,
michezo ya sinema na muziki. Hapo wengi ndio wanaotumbukia. Kaanza
Yahudi na watu wengine wakiwemo Waislamu wakafuatia.
Hatari mbaya zaidi ni pale tunapoyaingiza hayo mambo yao
ya uzushi kwenye dini yetu tukitarajia kwamba tunapata thawabu ilihali
tunaingia kwenye maangamizo zaidi. Manaswara wakaanza kuitukuza dai la
siku ya kuzaliwa Yesu kwa ibada za kuvumbua na hatimaye leo tunawaona
wakibadili ibada hizo kwa matendo ya uzinzi, pombe, kamari na israfu.
Nao
Waislamu wametumbukia hapo hapo, kwa kuvumbua ibada ya Maulidi wakidai
kuitukuza siku inayodaiwa kazaliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam). Hakuna shaka yoyote kwamba Maulidi ni mwigo wa
Manaswara na tusipokuwa makini, vizazi vyetu vitakuja kusherehekea siku
hiyo kwa uzinifu, pombe, kamari na israfu.
Akili
inakuwa haielewi pale mtu mwenyewe anaposhindwa kusherehekea siku yake
ya kuzaliwa, vikaja vizazi vya karne za baadaye wakaanza kuisherehekea
siku yake. Ni ajabu kweli kweli. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam) alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo alizaliwa yeye. Kama
aliielewa siku ya kuzaliwa (ambayo ni Jumatatu) kwanini ashindwe
kuifahamu tarehe yake akaanza kuitukuza kwa kuwakusanya Maswahaba
wakaanza kusoma hayo Maulidi?
Na
vipi wasilione hilo kina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy na
Maswahaba wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambao hakuna anayewashinda
kwa mapenzi yao waliyokuwa nayo kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam)? Je, sisi tuna mapenzi ya Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwashinda watukufu hao? Basi kwanini wao
wasimsherehekee mazazi yake? Hatujiulizi hilo? Hatuna akili ya
kupambanua na kufikiri?
Haya
ni mambo yanayohitaji Muislamu kupambanua bila ya kupata taabu yoyote.
Tuangalie namna hayo Maulidi yanavyofanywa katika maeneo yetu ya
makaazi. Huanza kusherehekewa baada ya Swalatul-Ishaa hadi Alfajiri siku
ya pili. Mtindo huu unafanana kabisa na mkesha wa Krismasi unaofanywa
kanisani hadi siku hiyo ya Krismasi. Na kwani Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizaliwa usiku?!
Jengine
ni kwamba hapo panapofanywa hiyo sherehe kitaifa, ni sehemu ya ukanda
wa bahari. Kuna mkusanyiko wa wanawake na wanaume. Kwenye gubi gubi la
usiku, ni jambo gani litakalowazuia wasizigeuze fukwe za bahari kuwa ni
vitanda vya sita kwa sita?
Mara
kadhaa Maulidi yamekuwa yakifanyika ndani ya kumbi za pombe au tamasha
za muziki. Huenda ikawa sio kwa kuadhimisha kuzaliwa Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini Maulidi ya kusherehekea
harusi, matamasha ya muziki au siku za kuzaliwa baadhi ya Waislamu huwa
zinaadhimishwa ndani ya kumbi hizi. Ibada ya kweli kweli haitakubali
kushirikishwa ndani ya kumbi hizi.
Hayo
ndio Maulidi ambayo wengi wao wanaamini kuwa ni ibada. Na kuna hoja
nyingi zenye ushahidi wa Qur-aan na Sunnah zilizokusanywa ndani ya
alhidaaya zitakazomtosheleza Muislamu kutosherehekea siku hiyo.
Chapisha Maoni