Nani Masiyhud-Dajjaal? Ni Mtu Au Jini? Ataingia Kila Kona Ya Dunia?

0 coment

SWALI


Assalamualaikum Warahmatullahi Wa Barakatuh,

Ni matarajio yangu kuwa nyote katika Alhidaaya ni wazima wa afya na mko tayari kutupatia mafundisho/ ukumbusho juu ya mambo yanayohusu dini yetu ya uislam. Nimewahi kusikia mawaidha kutoka kwa sheikh mmoja juu ya kiumbe anayeitwa  Dajjal  na vituko vyake, na hata tukausiwa na  Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa katika swala zetu tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu atuepushe  na vituko vya huyo dajjal.

Swali langu ni kuwa huyu dajjal ni mtu au ni jinni na je huyo dajal atatembea kila kona ya dunia hii?
Wabillah ttaufiyq

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Masiyhid Dajjaal. Hakika ni kuwa kila Nabii na Mtume aliyetumwa hapa ulimwenguni pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuonya kuhusu kiumbe huyu ambaye umemuulizia. Hiyo ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"Ninawatahadharisha naye kama vile Nabii Nuuh alivyowatahadharisha watu wake" (al-Bukhaariy na Muslim).
Na pia,
"Hakuna Mtume aliyetumwa isipokuwa amewatahadharisha watu wake na mwenye jicho moja mrongo" (al-Bukhaariy na Muslim).

Hebu tutazame baadhi ya sifa ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia kuhusu Dajjaal ili tuwe na taswira nzuri kumhusu. Huu ni ufupisho wa Hadiyth kadhaa ambazo zinapatikana katika Swahiyh al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim). Nazo ni kama zifuatazo:

  1. Atakuwa na jicho moja tu la upande wa kushoto, na kutokuwa na jicho la kuliani. Jicho lenyewe litakuwa kama zabibu inayoelea.
  2. Kati ya macho yake pameandikwa neno "kafiri".
  3. Atakapotokeza atakuwa na maji na moto. Kinachoonekana ni moto basi hayo ndio maji baridi ama kile watu watakachokiona ni maji baridi basi huo ni moto unaounguza.
  4. Hatoweza kuingia miji miwili mitukufu, nayo ni Makkah na Madiynah.
  5. Atapatiwa muujiza wa kuweza kumuhuisha aliyekufa.
  6. Atashindwa kumuua mwenye Imani thabiti.
  7. Hatokuwa na kizazi.
  8. Wafuasi wake watakuwa ni Mayahudi.
  9. Atauliwa na Nabii 'Iysa ('Alayhis Salaam) katika lango la mji wa al-Lud (Palestina).

Ama mtu huyu kuweza kuzunguka ulimwengu mzima hakuna ajabu kwani uwezo huo atapewa na Allaah Aliyetukuka naye atakuwa ni mtihani mkubwa kwa watakaokuwa hai wakati huo.

Qur-aan inatueleza kuwa Dhul Qarnayn naye alipatiwa na Allaah Aliyetukuka uwezo wa kutembea sehemu nyingi kama Anavyotuambia Allaah Aliyetukuka. Tafadhali tazama Qur-aan 18: 83 – 99.

Na Allaah Anajua zaidi

Share this article :

Chapisha Maoni

 
Designed By AL HUDDAH
Islamic foundation
Copyright © 2013. RIAD BIN RUWEHY | All Rights Reserved