Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa ambayo hayasambazwi kwa mtu
mwingine kwa kuwa hakuna vimelea mwilini vinavyohusiana na magonjwa
hayo. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kama ya moyo na mishipa ya damu,
figo, saratani, kifua sugu, kisukari, magonjwa ya akili na mengine ya
kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell Disease).
Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya 2013,
inadai magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio chanzo kikubwa cha vifo
ulimwenguni, yakifanya asilimia 63 ya vifo vyote kwa mwaka. Magonjwa
yasiyo ya kuambukiza huua watu zaidi ya milioni 36 kila mwaka. Asilimia
80 ya vifo vinasababishwa na magonjwa hayo hutokea nchi zinazoendelea,
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo. Inakisiwa kuwa mwaka 2020
magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza yatasababisha asilimia 73 ya vifo
vyote duniani na asilimia 60 ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.
Nchini Tanzania, katika mpango wa upimaji wa afya kwa magonjwa
yasiyoambukiza jijini Dar es Salaam, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) umebaini kuwa idadi kubwa ya wanaume wanapatwa na magonjwa hayo
kuliko wanawake. Uchambuzi huo umeonyesha magonjwa yasiyoambukiza kama
kisukari, shinikizo la damu na saratani zote ambazo zimekuwa chanzo cha
vifo hivyo, huku serikali ikisema imeamua kuongeza juhudi za makusudi
kupambana nayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mfuko wa Bima ya Afya, athari ya magonjwa
yasiyoambukiza ni mara nne zaidi ya watu waliopo mijini kuliko vijijini,
huku asilimia 12.8 ya wanaougua wakiwa wako mijini na asilimia 3.1 wako
vijijini kutokana na mfumo wa maisha.
Uchunguzi mwingine uliofanywa na jopo la madaktari bingwa kuanzia mwaka
2011 hadi 2014 ulibaini asilimia 79 ya watanzania wazee waligundulika
kuugua magonjwa ya kisukari, macho na shinikizo la damu. Pia walidai
magonjwa hayo yamekuwa kikwazo cha maendeleo kutokana na kuwasumbua
wazee na hata wenye umri wa kati ya miaka 40 na 50.
Kisukari ikiwa ni moja ya muuaji wa kimya kimya katika kundi hili la
magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Watu milioni 285 duniani kote
wameathiriwa na kisukari ambayo ni sawa na asilimia 6.6 ya idadi ya watu
wote ulimwenguni pia ikishika nafasi ya 5 kwa kusababisha vifo duniani.
Nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya watu wenye kisukari ni China
wagonjwa milioni 43.2, India wagonjwa milioni 40.9, Marekani wagonjwa
milioni 25.8, Urusi wagonjwa milioni 9.6 na Brazil wagonjwa milioni 6.
Nchi zenye idadi kubwa ya watu wazima wenye kisukari ni Nauru kwa
asilimia 30, Bahrain kwa asilimia 25.5, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)
kwa asilimia 25, Saudi Arabia kwa asilimia 23.7 na Mauritius kwa
asilimia 20.
KISUKARI NI NINI HASWA?
Sukari mwilini hutokana na vyakula pamoja na vinywaji tunavyotumia kila
siku na hutumika kuupa mwili nguvu. Glukosi ni aina ya sukari ambayo
huzipa chembe za mwili nishati. Hata hivyo ili glukosi iingie ndani ya
chembe hizo inahitaji insulini. Insulini ni kemikali (Homoni) ambayo
hutokezwa na kongosho (Pancrease).
Kisukari ni ugonjwa unaotokana na mtu kuwa na sukari nyingi kupita
kiasi kwenye damu. Ugonjwa huo huvuruga utaratibu wa kuingiza sukari
ndani ya chembe kutoka kwenye damu kwa kuwa chembe huhitaji sukari ili
kupata nishati.
Ugonjwa wa Kisukari hutokea pale ambapo tezi ya kongosho inaposhindwa
kutengeneza kichocheo (Homoni) aina ya insulin au pale mwili
unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho na kusababisha kuongezeka
kwa sukari (Hyperglycemia) au kushuka kwa kiwango cha sukari
(Hypoglycemia). Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababishwa na kuwa na
kiwango kidogo cha insulin mwilini, mwili kutosikia kichocheo hicho au
yote mawili.
TAKWIMU MBALIMBALI ZA UGONJWA WA KISUKARI
Kulingana na ripoti mbalimbali karibu watu milioni 316 ulimwenguni pote
wana kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu, ingawa wengi wao hawajui
wana kiwango hicho. Kwa mfano, nchini Marekani pekee asilimia 90 ya watu
wenye sukari nyingi kwenye damu hawatambui kama wana tatizo hilo.
Ingawa asilimia 8.3 ya watu watu wa Marekani wana Kisukari ambayo ni
sawa na watu milioni 25.8 na kufanya Kisukari cha 7 kusababisha vifo vya
watu Marekani.
Mamilioni ya watu wana ugonjwa huo lakini hawana habari! Ni ngumu zaidi
kutibu ugonjwa wa kisukari kwa kuwa mtu anaweza kuishi nao kwa muda
mrefu kabla haujagunduliwa. Hiyo ndiyo sababu watu husema kwamba ugonjwa
huo huua kimyakimya.
NINI CHANZO HASA CHA KISUKARI?
Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna
chakula kinavyovunjwa vunjwa na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu.
Wakati chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea. Moja ni sukari
inayoitwa glucosi ambayo ni chanzo cha nishati/nguvu mwilini huingia
katika damu. Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho (Pancrease)
kutengeneza kichocheo cha insulini. Kazi ya insulini ni kuondoa glucosi
katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako
hutumika kama nishati.
Watu wenye kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu
kuliko inavyotakiwa kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye
seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha
nguvu. Hii ni kutokana na moja ya sababu zifuatazo, huenda kongosho zao
haziwezi kutengeneza insulini ya kutosha au seli za mwili wao
haziathiriwi na insini kama inavyotakiwa au sababu zote hizo mbili.
Kama wewe ni mnene kupita kiasi, hufanyi mazoezi kwa ukawaida au una
watu wa ukoo walio na kisukari, huenda tayari una kiwango cha juu cha
sukari kwenye damu. Ongezeko la sukari kwenye damu mbali na kuwa
kisababishi cha kisukari, hali hiyo inahusianishwa na hatari ya kupatwa
na ugonjwa wa akili uitwao 'DEMENTIA'.
Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa wa kisukari. Lakini lazima
tuseme kwamba kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza
uzito wa kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi
tofauti. Ugonjwa wa kisukari umeitwa kwa kufaa "ugonjwa unaoathiri kiini
cha nishati ya mwili". Mwili unaposhindwa kutumia glukosi, mifumo
mbalimbali ya mwili inaweza kuacha kufanya kazi au hata kusababisha
kifo.
Ugonjwa wa Kisukari kitaalamu hujulikana kama 'DIABETES MELLITUS'. Jina 'Diabetes Mellitus'
linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha 'kunyonya' na neno la
Kilatini linalomaanisha 'tamu kama asali'. Maneno hayo yanafafanua
vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na
ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye
njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe mkojo huwa na ladha
tamu kwa kuwa una sukari. Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za
kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa
kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha
sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo basi hilo lilimaanisha
kwamba mkojo una sukari.
NI NANI ANAWEZA KUWA NA UGONJWA WA KISUKARI?
Watu walio katika makundi yafuatayo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kisukari:-
– Wenye uzito uliozidi,
– Wenye historia ya kuwa na wagonjwa wa kisukari katika familia zao,
– Wanawake waliozaa watoto wenye kilo 4 au zaidi,
– Watu wasiojishughirisha au wasiofanya mazoezi,
– Wenye shinikizo la damu,
– Wenye msongo wa mawazo na
– Wenye matumizi makubwa ya pombe na sigara.
Watu hawa wanashauriwa kupima sukari yao kila mwaka wakiwa na umri wa miaka 45 na kuendelea.
Kuna hatari kubwa ya kuugua ugonjwa huo ikiwa mtu ana mafuta mengi
katika tumbo na kiuno chake kuliko katika mapaja yake. Mafuta katika
kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha sukari
kwenye damu.
Wavutaji wa sigara wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwani zoea hilo
hudhuru moyo na mfumo wa mzunguko wa damu na kubana mishipa ya damu.
Kitabu kimoja kinasema kwamba asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari
ambao hulazimika kukatwa viungo ni wavutaji wa sigara.
DALILI ZA UGONJWA WA KISUKARI
~ Kunywa maji mengi kuliko kawaida na kusikia kiu kila wakati.
~ Kwenda haja ndogo mara kwa mara. Watoto kukojoa kitandani.
~ Kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati.
~ Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri.
~ Kusikia njaa kila wakati na kula sana.
~ Wanawake kuwashwa ukeni.
~ Kutoona vizuri.
~ Kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake.
~ Ganzi, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole.
~ Miguu kuoza na hata kupata gangrini.
~ Kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu.
~ Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka.
~ Majipu mwilini.
~ Kwenda haja ndogo mara kwa mara. Watoto kukojoa kitandani.
~ Kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati.
~ Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri.
~ Kusikia njaa kila wakati na kula sana.
~ Wanawake kuwashwa ukeni.
~ Kutoona vizuri.
~ Kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake.
~ Ganzi, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole.
~ Miguu kuoza na hata kupata gangrini.
~ Kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu.
~ Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka.
~ Majipu mwilini.
Wenye dalili hizi wanashauriwa kupima sukari ili kubaini kama wana kisukari.
Chapisha Maoni