TAMKO LA TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI
WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA KAULI YA
MAASKOFU KUINGILIA MADARAKA YA BUNGE NA
KULITAKA LISIJADILI JUU YA MAHAKAMA YA KADHI
1. Hivi karibuni ndugu zetu, viongozi wenzetu wa
Dini ya Kikristo chini ya “mwamvuli” wa Jukwaa la
Wakristo Tanzania, wametoa Tamko la kuitaka
Serikali isitishe Mchakato wa Mahakama ya Kadhi
kwa kuondoa muswada wa Sheria ya Marekebisho
ya Sheria Mbalimbali Na. 02 wa Mwaka 2014
unaopendekeza, pamoja na mambo mengine,
kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Tamko la
Sheria ya Kiislamu, Sura ya 375(The Islamic Law
(Restatement) Act, Cap.375) na ambao unatarajiwa
kujadiliwa katika Mkutano wa 18 wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoendelea
hivi sasa Dodoma, ikiwa ni ahadi ya Serikali
iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo
Kayanza Pinda mwishoni mwa Mkutano wa Bunge
Maalum la Katiba.
2. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania imelipitia Tamko hilo la Jukwaa la
Wakristo Tanzania kwa umakini mkubwa na baada
ya tafakuri ya kina juu ya kadhia hii, Taasisi ya
Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania
inaweka bayana yafuatayo:-
3. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania imesikitishwa sana na Tamko la Maaskofu
chini ya Jukwaa la Wakristo Tanzania kuingilia kwa
hila madaraka ya Bunge na kutaka kuifanya
Serikali iliyotoa ahadi kupitia Mheshimiwa Waziri
Mkuu Mizengo Pinda ionekane imewadanganya
Waislamu ili Waislamu waichukie Serikali yao.
Ikumbukwe kwamba Ahadi ya Marekebisho ya
Sheria kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania
Bara ni Ahadi ya Serikali.
4. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania inawanasihi na kuwaomba Maaskofu
wawaachie “uhuru” Wabunge Waumini wa Dini ya
Kikristo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania waujadili muswada huo bila ya shinikizo
la kiimani la kuukataa.
5. Mbinu zozote za kuwashawishi Wabunge kiimani
kutekeleza Maazimio ya Maaskofu chini ya Jukwaa
la Wakristo Tanzania, huo ni “udini” ambao ni
hatari sana kwa Umoja na Mustakabali wa Taifa
letu.
6. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania inawakumbusha Maaskofu kwamba
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina
Vyombo vya Uchunguzi na Utafiti vyenye uwezo
wa kubaini maeneo yanayovunja Umoja wetu wa
Kitaifa, na hata mambo yanayopingana na Katiba
ya nchi yetu tuliyo nayo sasa na ile
inayopendekezwa. Kamwe Maaskofu si sehemu ya
vyombo hivyo. Ni vizuri wakaendelea kuongoza
Ibada na kazi hizo za Uchunguzi wakawaachia
walioaminiwa kuzifanya.
7. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania inachukua fursa hii kuwakumbusha
Maaskofu na Watanzania kwa ujumla kwamba
“Hofu” ya kuwepo Mahakama ya Kadhi Tanzania
Bara ni hofu “bandia”, kwani kesi zinazohukumiwa
kwa mujibu wa Sheria ya Kiislam zinazohusiana na
Ndoa ya Kiislamu, Talaka, Miirathi, Wasia, Waqfu na
Malezi ya Watoto zinapatiwa uamuzi (hukumu)
katika Mahakama zilizopo na kwa miaka kadhaa na
wala Maaskofu hawajapata kudai ziondolewe kwa
kuwa ni za kidini. Ieleweke kuwa wanachoomba
Waislamu ni kubadilishiwa Hakimu ili aje Kadhi
ambaye ana taaluma na uelewa mpana wa Sheria
ya Kiislamu. Je, ni vipi kasoro ya Dini ionekane
baada ya kuletwa Kadhi atakayezipatia hukumu za
kesi hizo na isionekane sasa wakati zipo
Mahakamani kwa Hakimu anayezikosea hukumu
hizo?
8. Kuhusu hofu ya Maaskofu kwamba, kwa kuwa
baadhi ya Taasisi za Kiislamu hazikubaliani na
Mamlaka ya Mufti wa Tanzania kwenye masuala
yao, na hivyo kuijumlisha hoja hiyo kama hoja ya
kutaka muswada huo uondolewe kwa ujumla
wake, tunapenda kuwakumbusha na kuwataka
viongozi wa kikristo wayaache mambo ya ndani ya
waislamu yashughulikiwe na waislamu wenyewe.
Kadhalika wakumbuke kauli yao “ Ya Kaizari mpe
Kaizari, na ya Mungu mpe Mungu” na hivyo basi
waiache Serikali na Bunge kutekeleza majukumu
yao bila ya kuingiliwa kiimani. Viongozi wa Kikristo
watambue kuwa Waislamu wanajua migongano na
mifarakano iliyopo ndani ya makanisa lakini
waislamu hawajathubutu kuyaingilia mambo ya
ndani ya wakristo kwa namna yoyote na
wamewaachia Wakristo watatue matatizo yao wao
wenyewe. Viongozi wa Kikristo waache
kuwadanganya Waislamu kwa “huruma ya
mamba” na ikiwa kweli Viongozi hawa wa Kikristo
ni wasikivu wa sauti ya Baadhi ya Taasisi za
Kiislamu wangefanyia kazi madai ya uwepo wa
“Mfumo Kristo” yaliyotolewa hadharani na Taasisi
hizo.
9. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania itashangazwa sana iwapo Serikali itaamua
kuuondoa Bungeni Muswada unaolenga
kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara kwa
kisingizio cha kupingwa na baadhi ya Taasisi za
Kiislamu na chembilecho itadhihirika wazi kuwa
Serikali imeuondoa Muswada huo kutokana na
shinikizo la Jukwaa la kikristo, kwa kuwa ni Serikali
hii iliyoamua kuendelea na mchakato wa SENSA
mwaka 2012 pamoja na kupingwa na baadhi ya
Taasisi za Kiislamu.
10. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania inawaomba Waheshimiwa Wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wazingatie viapo vyao vya kuitumikia nchi hii na
watu wake kwa uadilifu na bila ya kuathiriwa na
shinikizo la kiimani lililotolewa na Maaskofu kupitia
Jukwaa la Wakristo Tanzania waupokee Muswada
huo na waupime kwa hoja na kutoa majibu yenye
hoja, na kamwe wasikubali wagawanywe kiimani
kwani jaribio la kuligawa Bunge kiimani ni jambo la
hatari linalotishia kuligawa Taifa la Tanzania.
11. Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania haina pingamizi na dhamira ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwafahamisha
“wenye hofu” na uwepo wa Mahakama ya Kadhi
Tanzania Bara kuwa Mahakama hiyo haina
madhara yoyote kwa Umoja, Mshikamano na
Mustakabali wa Taifa la Tanzania. Taasisi ya
Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania
inaahidi kumpa ushirikiano wowote atakaouhitaji
katika utoaji wa elimu hiyo.
12. Mwisho, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa
Kiislamu Tanzania inawaomba Waislamu wote nchi
nzima kuwa watulivu na kuendelea kuiombea nchi
yetu isiingie katika machafuko yoyote.
Wabillah Tawfiiq.
Chapisha Maoni