Nimeona ni bora niandike makala hii ili
iweze kuwasaidia na wengine kujua nini
chanzo na mhusika afanye nini pale
anapopatwa na tatizo hili.
Maumivu wakati wa hedhi (period pains) au
kitaalamu dismenorrhea, ni maumivu
yanayojitokeza sehemu ya chini ya tumbo au
kiunoni wakati mwanamke anapoanza
kupata siku zake au kabla ya hapo.
Maumivu hayo huweza kuwa madogo au ya
wastani huku baadhi ya wanawake wakipata
maumivu makali sana. Maumivu hayo huanza
pale yai linapotoka katika mrija (fallopian
tube) na kuteremka chini ya mrija huo wakati
wa Ovulation.
AINA YA MAUMIVU
Maumivu ya tumbo la hedhi yapo ya aina
mbili. Ya kwanza ni maumivu yasiyokuwa na
sababu zozote za kimsingi za kitiba. Katika
aina hii maumivu ni ya kawaida na huhisiwa
sehemu ya chini ya tumbo na kiunoni.
Maumivu hayo huanza siku moja au mbili
kabla ya hedhi na humalizika baada ya siku
mbili au nne.
Aina ya pili ni yale maumivu
yanayojumuisha maumivu
yanayosababishwa na sababu nyinginezo za
kitiba kama vile matatizo katika kizazi,
ugonjwa wa nyonga (PID) na matatizo katika
mirija ya mayai.
Nusu ya wasichana na wanawake hupata
maumivu wakati wa hedhi na karibu asilimia
kumi mpaka kumi na tano wanasema kuwa
hupata maumivu makali.
Uchunguzi unaonesha kuwa kuna sababu
mbalimbali zinazoweza kuongeza
uwezekano wa kuumwa tumbo wakati wa
hedhi.
Sababu hizo ni kama kuwa na umri wa chini
ya miaka 20, kuvunja ungo wakati wa miaka
11 au chini ya miaka hiyo, kutoka damu
nyingi wakati wa hedhi, wanawake ambao
hawajawahi kuzaa.
Magonjwa yanayoweza kusababisha mtu
kupatwa na maumivu ya tumbo la hedhi.
Miongoni mwa magonjwa hayo ni:
Endometriosis. Hii ni hali ambayo seli za ndani
ya mfuko wa uzazi huanza kuoka nje ya fuko
hilo, au hata sehemu nyinginezo
Adenomyosis: Huu ni ugonjwa wa
wanawake ambapo tezi au uvimbe (tumors)
zinaota katika mfuko wa uzazi.
PID au Ugonjwa wa uvimbe katika
nyonga.
Magonjwa ya zinaa yanayotokana na
bakteria au magonjwa ya kuambukiza ya
zinaa.
Mlango wa uzazi unapokuwa mdogo kiasi
kwamba unazuia damu ya hedhi isitoke kwa
urahisi.
baadhi ya magonjwa yanayoweza
kusababisha mtu kupatwa na maumivu ya
tumbo la hedhi. niliishia kuelezea ugonjwa
wa uvimbe katika nyonga ambao
husababishwa na magonjwa ya zinaa
yanayotokana na bakteria au magonjwa ya
zinaa.
dalili za ugonjwa huo ni:
Maumivu kuja na kuondoka, kwa kiwango
tofauti (spasmodic).
Maumivu zaidi huwa sehemu ya chini ya
tumbo na huchanganyika na maumivu ya
sehemu ya chini ya mgongo ambayo
husambaa mpaka mapajani.
Kujihisi kutapika, kichefuchefu na wakati
mwingine hata kutokwa jasho.
Kupata choo laini au hata kuharisha na
wengine hufunga choo.
TUMBO KUWA KUBWA AU KUWA GUMU.
Kupata maumivu ya kichwa, kujisikia
kuchoka.
Kiwango cha maumivu ya tumbo la hedhi na
mchanganyiko wa dalili inategemea mtu na
mtu, mtu mwingine anaweza akawa anapata
karibu dalili zote nilizozitaja hapo juu na
mwingine ni baadhi tu au hata dalili moja.
Wanawake wengi hujitambua bila hata
msaada wa daktari.
USHAURI
Iwapo mwanamke atapata maumivu makali
sana ni bora akamuone daktari ili wafanye
vipimo kama vile Ultrasound, CT na CT-Scan,
MRI na vinginevyo ili kufahamu nini chanzo
cha maumivu hayo kuwa makali
MATIBABU
Matibabu ya maumivu ya tumbo la hedhi kwa
kawaida huweza kutibika kwa urahisi kwa
kutumia vidonge vya kupunguza maumivu,
kama vile Ibuprofen, naproxen au aina
nyinginezo za vidonge visivyokuwa na
steroids (NSAIDS). Pia kuna wakati madaktari
wanaweza kumshauri mgonjwa kutumia
vidonge vya kuzuia mimba, Vidonge hivyo
huzuia mzunguko wa yai au Ovulation na
kupunguza ukali wa maumivu ya tumbo la
hedhi.
Pia wanawake wanashauriwa kufanya
baadhi ya vitendo ambavyo hupunguza
maumivu hayo, kama kuoga maji moto,
kuweka kitambaa chenye joto katika sehemu
ya chini ya tumbo, kufanya mazoezi kama
yoga, meditation, kutumia vidonge vya
vitamin E, Thiamine na Omega 3 kumetajwa
kuwa husaidia katika suala hilo. Wanawake
wanaopatwa na matatizo kama
hayo ni bora wapumzike vyema na kupata
usingizi wa kutosha.
Vilevile unaweza kujiepusha na kupatwa na
maumivu ya tumbo la mwezi kwa kufanya
yafuatayo:
Kujitahidi kula matunda, mbogamboga na
kupunguza kula vyakula vyenye mafuta
mengi, pombe, kafeini, sodium na sukari,
kufanya mazoezi ya viungo, kujiepusha na
wasiwasi na mawazo na kuepuka kuvuta
sigara.
Chapisha Maoni