Wengi
miongoni mwa makhatibu wa Misikitini na wahadhiri wanainasibisha na
Swahaba Tha’alabah bin Haatwib (Radhiya Allaahu ‘anu) Aayah ya 75 ya
Surat At-Tawbah.
Katika Aayah hiyo Allaah Anasema:
"Na
miongoni mwao hao (wanafiki) wako waliomuahidi Allaah kuwa; "Akitupa
katika fadhila Zake tutatoa sadaka na tutakuwa miongoni mwa wanaotenda
mema. Lakini Alipowapa hizo fadhila Zake walizifanyia ubakhili na
wakakengeuka. Nao (mpaka hivi sasa) wanakengeuka. Kwa hivyo (Allaah)
Akawalipa unafiki (kuutia) nyoyoni mwao mpaka siku ya kukutana naye kwa
sababu ya kuhalifu kwao waliomuahidi Allaah na kwa sababu ya kusema kwao
uongo."
Kimetungwa
kisa kirefu kinachosema kuwa Tha’alabah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye
aliyekusudiwa katika aya hii kuwa alikataa kutoa Zakaah kumpa Mtume wa
Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kisa
kinasema kuwa Tha’alabah alikuwa masikini sana na kwamba alikuwa mwingi
wa kwenda Msikitini mpaka akapewa jina la kubandika akaitwa 'Njiwa wa
Msikiti'.
Kisa kinaendela kusema kuwa; Siku moja Tha’alabah alimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"Niombee
dua ili Allaah aniruzuku wanyama wengi sana." na Mtume wa Allaah
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea dua na idadi ya
kondoo wake ikaongezeka ikambidi atafute nyumba nje ya mji wa Madiynah.
Akawa haswali isipokuwa baadhi tu ya Swalah za fardhi.
Idadi
ya kondoo ikazidi kuongezeka na safari hii ikabidi asogee nje zaidi ya
mji wa Madiynah, na akawa hana tena wakati wa kuswali isipokuwa siku ya
Ijumaa tu.
Idadi
ya kondoo ikaongezeka tena akaacha kuswali hata hiyo Ijumaa, na Mtume
wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipompeleka
mjumbe wake kwa ajili ya kukusanya pesa za Zakaah, Tha’alabah akakataa,
akasema: "Hakuna Zakaah yenu katika mali yangu, mali hii ni yangu mwenyewe nimeirithi kwa babu zangu."
Kisa
kinaendelea kusema kuwa Tha’alabah alihisi vibaya akachukua mali ya
Zakaah na kuipeleka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) aliyeikataa mali hiyo. Na alipofariki dunia Mtume wa
Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Tha’alabah
alichukua mali ya Zakaah akamuendea Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu),
akamuambia: "Chukua",
lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaikataa akamwambia: "Siwezi
kukubali alichokikataa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam)."
Akaipeleka
kwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye pia akasema: "WaLlaahi siwezi
kukubali alichokikataa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi
wa sallam)."
Kisa
hiki si cha kweli na isnadi yake ni ya kupangwa, juu ya kuwa
kimesimuliwa na Ma’ulamaa wakubwa kama vile Ibn Kathiyr na Ibn Jariyr na
Ibn Athiyr, na hii ni kwa sababu zifuatazo:
1. Allaah Hakatai toba ya mja Wake.
Allaah Anasema
"Wakitubu wakasimamisha Swalah na wakatoa Zakaah basi iacheni njia yao (waacheni)." At-Tawbah: 5.
Na Akasema:
"Sema:
"Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya
Allaah. Bila shaka Allaah Husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwingi wa
kusaheme dhambi (na) Mwingi wa kurehemu." Az-Zumar: 53.
Aayah
zilizotangulia zinatujulisha kuwa hata mshirikina akitubu basi Allaah
Ataikubali toba yake, itakuwaje basi Aikatae toba ya Muislamu aliyeacha
kutoa Zakaah?
2. Anasema Imaam Al-Qurtwuby katika Jaami’ al-Ahkaam:
“Tha’alabah
alipigana vita vya Badr, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) alishuhudia kuwa ni Muislamu wa kweli, kwa hivyo kisa
hiki anachonasibishwa nacho si cha kweli.
3. Anasema Al-Haafidh Al-‘Iraaqiy katika tahakiki ya Hadiyth za kitabu cha Al-Ihyaa ‘Uluum ad-Diyn cha Ghazaliy:
“Hadiyth hii imetolewa na Atw-Twabaraaniy na isnadi yake ni dhaifu”
4. Anasema Ibn Hajar katika Al-Iswaabah Fiy Tamyiiz asw-Swahaabah:
“Kisa hiki sidhani kama
ni sahihi kwa sababu Tha’alabah huyu amepigana vita vya Badr, na
Hadiyth sahihi ya Mtume wa Allaah inasema kuwa; Waliopigana vita vya
Badr hawaingii motoni, na kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) aliwaambia; “Fanyeni mtakacho, mumekwisha
ghufuriwa madhambi yenu.
Aliyefikia daraja hii itakuwaje awe mnafiki kama inavyoeleza Aayah?”
5. Na
katika Fatwa za Kamati ya kudumu ya Utafiti wa Kielimu na Utoaji Fatwa
chini ya Wanachuoni ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah Aal Ash-Shaykh, Shaykh
‘Abdullaah bin Ghudayaan, Shaykh Swaalih Al-Fawzaan na Shaykh Bakr Abu
Zayd, imeelezwa:
“Kilichopokelewa kuhusu sababu ya kushuka kwa Aayah:
“Na miongoni mwao hao (wanafiki) wako waliomuahidi Allaah kuwa; "Akitupa katika fadhila Zake...” At-Tawbah: 75,
kuwa ni Tha’albah bin Haatwib – sanadi yake si sahihi-, na
Tha’alabah bin Haatwib ni Answaariy aliyeshiriki vita vya Badr,
akafariki Shahidi katika vita vya Uhud, kama walivyothibitisha
Wanachuoni kadhaa miongoni mwao ni Al-Haafidh Ibn Hajar (Allaah
Amrehemu).
‘Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah Lil-Buhuuth al-‘Ilmiyah wal Iftaa’ (49/26).
6. Amesema Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu), kauli Yake Allaah:
“Na miongoni mwao hao (wanafiki) wako waliomuahidi Allaah...” na
Aayah zenye kuendelea kuwa zimeshuka kwa ajili ya wanafiki. Na kuwa
habari zilizo maarufu kuwa Aayah hizo zimeshuka kumhusu Tha’alabah bin
Haatwib katika kisa kirefu ambacho wamekitaja wafasiri wengi na wakawa
wahadhiri na watoaji mawaidha wanakieleza sana –ni kisa dhaifu hakina
usahihi- , na kinapingana na lile linalojulikana kuwa ni jambo la lazima
katika dini kulifahamu, kwamba Allaah Anapokea Tawbah ya mwenye kutubia
kwa dhambi yoyote ile atakayoifanya.”
Sharh ‘Uswuul fiy Tafsiyr’ Ibn ‘Uthaymiyn.
Chapisha Maoni