Hijaab

0 coment

Salamu pwani na bara, zivuke kote angani,
Kwa watu wenye busara, nina kidogo maoni,
Hamtapata hasara, dakika chache nipeni
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Ni vazi lenye sitara, inasitiri usoni,
Inakuweka imara, kwa kushika yako dini,
Hakuna wa kukukera, umemshinda shetani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Hijaab kuwajibika, ipo kwenye Qura’ani, (Al-Ahzaab 33:59)
Hakika walisifika, wanawake wa zamani,
Na tena huheshimika, wapitapo mitaani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Usionyeshe uzuri, unapotoka nyumbani,
Hii ndio dasturi, Ameiweka Manani, (An-Nuur 24:31)
Mwili unapositiri, unaonyesha imani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.
Ukijipamba usoni, kutoka wazi njiani,
Na marangi mdomoni, na wanja tele machoni,
Watu watakutamani, wakufuate hadharani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Kila kitu cha thamani, kinafichwa kwa makini,
Na mwili una thamani, Kauumba Wa mbinguni,
Binadamu tazameni, sio kama hayawani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Hijaab ndio twahara, utakaso kwa yakini,
Haifai kujipara, kuzunguka madukani,
Mwili sio biashara, kama bidhaa sokoni,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Hata unapozungumza, nyuma pale mlangoni,
Itabidi kuikaza, sauti sio laini,
Wasije watu kuwaza, kwa mawazo ya kihuni,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Vaa jalalibu pia, vizuri jifunikeni, (An-Nuur: 31)
Sema nyuma ya pazia, ukisema na mgeni, (Al-Ahzaab: 53)
Mungu Kaweka sheria, waifuate waumuni,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Ona mafuta mazuri, na marashi ya nguoni,
Hiyo hakika ni shari, ni fitina ya puani,
Watu watakufikiri, unawaita fuateni,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Baibui za mapambo, zitokazo Arabuni,
Zenye nakshi za urembo, zimekuwa ni “fasheni”,
Tulishasema kitambo, hazifai asilani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Mume wako peke yake, umpambie mwilini,
Kwa mapambo ujiweke, umvutie machoni,
Upate mapenzi yake, mume awe burudani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Toka nae ukitoka, yupo nawe ubavuni,
Mola Apate ridhika, Awabariki nchini,
Mpate Zake baraka, mwisho wake ni peponi,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Nawaomba dada zangu, wasifuate za kigeni,
Khasa zile za kizungu, ni mavazi ya shetani,
Watajuta “Ole wangu”, mwisho wake ni motoni,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Dunia ni matembezi, tupo hapa safarini,
Ametuumba Mwenyezi, na kutupa mitihani,
Hutuona waziwazi, huku tunafanya nini ?
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Kumbuka dada kaburi, na sanda pale shimoni,*
Umeyaacha mazuri, mikufu na mahereni,
Ona mwisho wa kiburi, ni kuoza mchangani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

Hapa ndio kaditama, nimefika ukingoni,
Tuikumbuke Kiyama, siku hiyo ya huzuni,
Sote tutaposimama, Mbele Yake Rahmani,
Hijaab kwa wanawake, ni vazi lenye sitara.

*
Share this article :

Chapisha Maoni

Designed By AL HUDDAH
Islamic foundation
Copyright © 2013. RIAD BIN RUWEHY | All Rights Reserved